top of page
Search

NERL Kutinga Raundi ya 36, Kariobangi Legends Youth Ikiendea Pointi 3

  • heartmediak4
  • Aug 2, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 02 Agosti 2024


NGARAMBE ya FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) wikendi hii (Jumamosi tarehe 3 Agosti na Jumapili tarehe 4 Agosti) itaingia raundi ya 36 ambapo michuano 12 imepangwa kuchezwa kwenye viwanja tofauti. Maafande wa Gunners na UEFA Despanol kila moja itakuwa mbioni kuwinda ushindi wa pointi sita baada ya kushiriki mechi mbili.



Jumamosi hii Gunners ya kocha, Brian Kaka itakuwa katika uwanja wa kiamboni kukaribisha UEFA Despanol kisha Jumapili itaialika Lula FC. Nayo UEFA Despanol Jumapili itashiriki mechi ya pili dhidi ya Umoja Rhinos ugani Tumaini Primary.

''Tunalenga kujitahidi kwa udi na uvumba kuhakikisha tunashinda mechi zote mbili na kujiongezea alama muhimu kwenye kampeni zetu,'' anasema kocha wa Gunners. Anashikilia kuwa kikosi chake kinajumuisha vijana wanaotosha mboga kulipua wenzao.

Nayo Ruai United imepangwa kukabili Babadogo United ugani Muhuri Muchiri.

Raui United itashuka dimbani ikiumiza majeraha ya kubamizwa kwa mabao 2-0 na Kariobangi Legends Youth wiki iliyopita. ''Kusema ukweli mechi hiyo haitakuwa mteremko wapinzani wetu sio wachache lakini tumefanya mazoezi ya kutosha tunaamini tutawashika shingo,'' anasema Joseph Maina nahodha wa Ruai United.


Anaongeza kuwa wanatamani sana kunyamazisha wapinzani wao ili wazidi kujiongezea tumaini la kumaliza nafasi nzuri. Ruai United inajivunia wachezaji kama Joseph Maina (nahodha), James 'Mau' Kamau, Steve Masayi, Martin Ekitela na Wilson Chege. Ruai United inashikilia nafasi ya 14 kwa kuzoa alama 38, mbili mbele ya Hakati Sportiff baada ya kushuka dimbani mara 34 na 35 mtawalia.

Nayo Kariobangi Legends Youth ya makocha, Geoffrey Wangalwa na Jeremiah Akhayo Jumamosi hii itakuwa ugenini ugani Jacaranda kukabili wenyeji wao Tumaini FC. ''Katika mpango mzima tutaendea ushindi wa alama tatu ili kuendelea kujiweka pazuri kunasa tiketi ya kupandishwa ngazi muhula ujao,'' anasema kocha mkuu. Anaongeza wamepania kuhakikisha wanashinda mechi zijazo ili kufungia wapinzani wao Lucky Summer wanaokuja kwa kasi sio haba.



Kariobangi inapigiwa chapuo kuendeleza mtindo wa kugawa dozi dhidi ya wapinzani wao kwa kuzingatia ndiyo timu ya pekee ambayo imepoteza mechi chache kabisa.

Kariobangi imeshiriki mechi 33, ambapo imeshinda patashika 27, imetoka nguvu sawa mara nne na kudondosha michuano miwili. Timu hiyo inajivunia wachezaji wepesi kama Victor Kinyuli, Bramuel Kasaya, George Karani, Ian Onyango (nahodha), Tom Bonfac, Dennis Wafula, Lawrence Otieno na Prise Luvutse Kati ya wengine. Prise Luvutse ni mchezaji anayekuja kiana kwani anazidi kuonyesha soka ya haiba ya juu.

Nayo Lucky Summer itacheza Jumapili dhidi ya Soweto All Stars ugani Jacaranda. ''Tumepania kushiriki mechi hiyo tukiwa makini zaidi maana hatutaki kudondosha alama yoyote kwenye mechi zijazo,' anasema Dan Nguya kocha wa Lucky Summer.

Kwenye mfululizo wa mechi za Jumapili, Santos Hotspurs imepangwa kucheza na Utawala Youth, Hakati Sportiff itachuana na Mathare North Youth, Mathare North United itakabili Rada Sports huku Gor Mahia Youth ikimenyana na Pumwani Sports. Automech FC itakwaruzana na Tena United huku Fortune Kinderen FC ikikutanishwa na Wendani All Stars.



Katika msimamo wa kipute hicho, Kariobangi Legends Youth inaongoza kwa kuzoa alama 85, nayo Lucky Summer ya pili kwa kusajili pointi 74, tano mbele ya Utawala Youth inayofunga tatu bora. Babadogo imetua nafasi ya nne kwa alama 68, sita mbele ya Automech FC.

 
 
bottom of page