NERL: Kariobangi Legends Youth Yanusia Ligi ya Taifa Daraja la Pili
- heartmediak4
- Jul 29, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumatatu, 29 Julai 2024.

KARIOBANGI Legends Youth imevuna pointi sita baada ya kucheza mechi mbili wikendi, Jumamosi na Jumapili tarehe 27 na 28 Julai kwenye kampeni za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL). Kariobangi ya makocha, Geoffrey Wangalawa na Jeremiah Akhayo imesajili ushindi wa mabao 2-0 kila moja dhidi ya Umoja Rhinos na Ruai United.
Kufuatia ufanisi huo Kariobangi imejiongezea tumaini la kunasa tiketi ya kupandishwa ngazi moja kwa moja kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao. Nayo Lucky Summer inayokamata nafasi ya pili chini ya kocha Dan Nguya imezaba UEFA Despanol mabao 2-0 kisha kutoka nguvu sawa bao 1-1 na Tena United.
Kwenye mechi ya Umoja Rhinos, Kariobangi ilibeba ushindi huo kupitia Ian Onyango na Bramuel Kavaya. Kwenye mechi ya pili, Dennis Wafula na Bramuel Kavaya kila mmoja alitikisa wavu mara moja. ''Ni kazi nzuri tunayofanya maana tunataka kubeba ubingwa na kupandishwa ngazi,'' anasema kocha wa Kariobangi. Anaongeza kuwa wamepania kutenda kweli kwenye mechi zilizosalia.
Lucky Summer ilizima wapinzani wao UEFA Despanol kupitia Dennis Opiyo na Rijkaard Lwa Otieno waliotupia kimiani bao moja kila mmoja. Kwenye patashika ya pili, Dennis Opiyo aliibuka shupavu kwa kutikisa wavu mara moja na kuisaidia kubeba alama moja. ''Bila shaka tunahitaji kushinda mechi zote zijazo ili kutimiza azma yetu kubeba taji la msimu huu ambapo sina shaka kutaja kuwa tuna mtihani mgumu,'' anasema kocha wa Lucky Summer. Anaongeza kwamba endapo watalemewa kubeba ubingwa wamepania kumaliza kati ya nafasi mbili bora ili kupanda ngazi nafasi ikipatikana.

Kwenye mechi hiyo Tena United ilipata bao hilo kupitia juhudi zake Kelvin Mwangi. Kabla ya mechi hiyo, Tena United ilikuwa imekung'uta Wendani All Stars kwa magoli 5-1. Fanuel Chibole na Kelvin Mwangi kila mmoja alishusha kimiani mabao mawili huku Lenox Madengwa akifunga goli moja.
Naye Bernard Mutisya alicheka na wavu mara moja na kubeba Tumaini FC kuadhibu Utawala Youth kwa bao 1-0 , hata hivyo kwenye mechi ya pili Tumaini ililala kwa bao 1-0 mbele ya Lula FC. Nayo Utawala Youth ambayo hunolewa na kocha, Bill Oporia ilinyuka Gunners mabao 2-1.
Kwenye mfufulizo wa matokeo ya Jumamosi, Automech FC na Soweto All Stars kila moja ilitoka nguvu sawa bao 1-1 mbele ya Pumwani Sports na Babdogo United mtawalia. Nazo Fortune Kinderen na Ruai United zilisajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Mathare North United na Lula FC mtawalia. Rada Sports na Gor Mahia Youth kila moja ilizoa mabao 2-2 mbele ya Santos Hotspurs na Mathare North Youth mtawalia huku Hakati Sportiff ikiagana bao 1-1 na Gunners.

Kwenye matokeo ya Jumapili, UEFA Despanol na Mathare North Youth kila moja ilisajili mabao 2-0 dhidi ya Soweto Allstars na Rada Sports mtawalia. Utawala Youth ilicharaza Gunners mabao 2-1, Santos Hotspurs ilikomoa Hakati Sportiff mabao 3-0, Babadogo United ilirarua Umoja Rhinos kwa magoli 4-1.
Automech ilinyamazisha Wendani Allstars kwa mabao 2-1, Fortune Kinderen ilipigwa bao 1-0 na Pumwani Sports huku Mathare North United ikitoka sare tasa dhidi ya Gor Mahia Youth.
Kutokana na matokeo hayo, Kariobangi Legends Youth inaongoza kwa kuzoa alama 85, nayo Lucky Summer ya pili kwa kusajili pointi 74, tano mbele ya Utawala Youth inayofunga tatu bora. Babadogo imetua nafasi ya nne kwa alama 68, sita mbele ya Automech FC.



