NERL: Kariobangi Legends Youth Kama Moto Nyikani
- heartmediak4
- Aug 6, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 6 Agosti 2024

KAMWE Kariobangi Legends Youth haitaki mzaha kwenye kampeni za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) msimu huu. Wachana nyavu hao wamenasa ushindi wa 28 kwenye mechi zilizochezwa Jumapili tarehe 3, Agosti na kuendelea kutetemesha wapinzani wao. Kila ushindi kwa wachezaji hao ni hatua nzuri inakoelekea kumaliza kileleni kwenye ngarambe ya msimu huu na kubeba tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao.
Kariobangi chini ya makocha, Geoffrey Wangalwa na Jeremiah Akhayo ilipata mtihani mgumu mbele ya wenyeji wao, Tumaini FC ugani Jacaranda na kufanikiwa kubeba ufanisi wa bao 1-0 lililotupiwa kimiani na Bramwel Kavaya. ''Bila shaka tunaendelea vyema kwenye kampeni zetu wala hatuna hofu maana tunaamini tutatimiza azma yetu kuibuka mabingwa na kusonga mbele,'' anasema kocha mkuu. Anaongeza kuwa wamepania kuendelea kujituma kwa udi na uvumba kwenye mechi zijazo kuhakikisha wanafungia wapinzani wao. Kariobangi Legends imekuja kwa kasi sio haba kwa kuzingatia ilianzisha mwaka uliyopita.

Nao mahasimu wao wa karibu, Lucky Summer ya kocha, Dan Nguya ilirarua Soweto All Stars kwa magoli 3-1 na kuendelea kujiongezea tumaini la kumaliza nafasi ya pili pia kujiweka pazuri kupandishwa daraja. Lucky Summer ilipata bao la kwanza baada ya mchezaji wa Soweto kujifunga. Kisha Joel Arika alifunga mabao hayo mengine. ''Buda kazi bado. Tumepania kupambana hadi mchezo wa mwisho ndiyo tutakubali yaishe endapo wapinzani wetu watamaliza kifua mbele,'' anasema kocha wa Lucky Summer.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Babadogo United ilitia kapuni alama tatu ilipoangusha Ruai United kwa mabao 2-1. Dan Simiyu na George Mukavana wa Babadogo United kila mmoja alicheka na wavu mara moja. Naye Martin Ekitela alifungia Ruai bao la kufuta machozi. James Kanyi alitikisa wavu mara moja na kusaidia Tena United kutoka nguvu sawa 1-1 dhidi ya Automech FC. Goli la Automech lilijazwa kimiani na Kelly Ndululu.
Kufuatia matokeo hayo, Kariobangi Legends Youth inaongoza kwa kuzoa alama 88, nayo Lucky Summer inashikilia nafasi ya pili kwa kusajili pointi 77 sita mbele ya Babadogo United. Utawala Youth inafunga tatu bora kwa alama 69, sita mbele ya Automech FC.


