NERL: Kariobangi L.Youth, Lucky Summer Mambo Mbaya
- heartmediak4
- Jun 26, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 25 Juni 2024.
TIMU ya Kariobangi Legends Youth na Lucky Summer FC kila moja inaonyesha imepania kupambana mwanzo mwisho kwenye mechi za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) msimu huu.
Vikosi hivyo vinazidi kupepea katika jedwali la kipute hicho baada ya kuvuna vinono kwenye mechi zilizochezwa wikendi ya tarehe 22 na 23 Juni 2024.
Hakika wachezaji wa timu hizo kamwe hawataki nyenyenye ligini. Kariobangi iliendeleza ubabe wake ilipoadhibu Lula FC kwa mabao 7-1 nayo Lucky Summer ilibeba magoli 8-0 mbele ya Rada Sports.
Wafungaji wa Kariobangi walikuwa Bramwel Kavaya na George Karani magoli mawili kila mmoja. Nao Ian Onyango (nahodha), Fidel Mwanzia na Laurence Otieno kila mmoja alicheka na wavu mara moja.
''Licha ya kupata ushindani mkali tupo ng'ang'ari kwenye kampeni za muhula huu,'' anasema kocha wa Kariobangi, Geoffrey Wangalwa. Anaongeza kuwa hakuna mteremko kipute cha muhula huu kinashusha upinzani wa kufa mtu.
Lucky Summer ilipata ushindi huo kupitia juhudi zake Joel Arika, Rijkaard Lwa Otieno na Levi Odede waliotikisa wavu mara mbili kila mmoja. Nao Dennis Opiyo na Ray Otieno kila mmoja alitupia kimiani bao moja.
''Napongeza wachezaji wangu kwa kazi nzuri wanayofanya kwenye kampeni za msimu huu,'' anasema kocha wa Lucky Summer, Dan Nguya. Anashikilia kuwa wachana nyavu wake wamefufua mchezo wao ambapo wameonyesha hakuna kulaza damu dimbani.
Nayo Babadogo United na Automech FC zilibeba mabao 4-1 na 4-0 mbele ya Utawala Youth na Ruai United mtawalia. Alex Ochieng wa Babdogo aliachia kombora mbili huku Winston Mang'oli na Dancun Chakali kila mmoja akitikisa wavu mara moja.


