NERL: Kariobangi Kupambana Hadi Kieleweke
- heartmediak4
- Jul 9, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 09 Julai 2024

KARIOBANGI Legends Youth imepania kupambana mwanzo mwisho kwenye michuano ya FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL).
Kocha wake, Geoffrey Wangalwa amedokeza baada ya Lucky Summer FC kuzaba Hakati Sportiff kwa mabao 6-1 na kuendelea kupunguza pengo lililopo kati ya vikosi hivyo. ''Kamwe hakuna kulaza damu mzigoni bali tutajituma hadi mechi ya mwisho tuhakikishe tumetwaa tikiti ya kupandishwa ngazi,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kwamba vijana wake wamo imara licha ya kuonekana kuteleza kwenye mechi kadhaa za hivi karibuni.

Kariobangi ndio imepoteza mechi chache kabisa maana hadi sasa imedondosha patashika mbili na kutoka nguvu sawa mara nne. Kariobangi inategemea wachezaji wepesi kama Victor Kinyuli, Bramwel Kasaya, George Karani, Ian Onyango (nahodha), Tom Bonface na Lawrence Otieno Kati ya wengine.
Naye kocha wa Lucky Summer, Dan Nguya anaamini kuwa aste aste ndio mwendo kwani wanazidi kupunguza mwanya dhidi ya wapinzani wao. ''Ingawa mahasimu wetu wamecheza mechi chache kutuliko tunalenga kukaza buti zaidi,'' akasema. Kwenye mchezo huo, Dennis Opiyo na Joel Arika kila mmoja alifunga mabao mawili naye Victor Otieno na Rijkaard Lwa Otieno wakitikisa wavu mara moja kila mmoja.
Nao Patrick 'Kaka' Muchoki na Gadson 'Soja' Maina kila mmoja alitikisa wavu mara moja na kubeba Tumaini FC kusajili mabao 2-0 mbele ya Automech FC.
Fortune Kinderen ilinyukwa magoli 5-0 na Ruai United huku Santos Hotspurs ikitoka sare tasa na Pumwani Sports. Nao wachezaji wa Utawala Youth walizamisha UEFA Despanol kwa mabao 2-1.

Mechi nyingi zilisitishwa wikendi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha maeneo mengi katika Kaunti ya Nairobi. Kutokana na matokeo ya wikendi, Kariobangi Legends Youth ingali kifua mbele kwa alama 67, moja mbele ya Lucky Summer baada ya kushuka dimbani mara 27 na 30 mtawalia. Baada ya Utawala Youth kupiga mechi 31 inafunga tatu bora kwa alama 62. Babadogo United inashikilia nne bora kwa alama 61, sita mbele ya Automech FC baada ya kushiriki mechi 27 na 30 mtawalia.


