top of page
Search

NERL: Kariobangi Kuendea Pointi 3 Ili Kukaa Mkao wa Kula

  • heartmediak4
  • Aug 16, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 16 Agosti 2024.



KARIOBANGI Legends Youth wikendi hii inapigiwa chapuo kuibuka mabingwa wa kampeni za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) endapo itashinda mechi moja baada ya kushuka dimbani mara mbili.


Kariobangi ya kocha, Geoffrey Wangalwa na Jeremiah Akhayo Jumamosi hii tarehe 17 Agosti itakuwa ugenini kucheza na Santos Hotspurs ugani Kincar. Kisha Jumapili tarehe 18 Agosti itakuwa katika uga wa kiamboni,Kariobangi North Primary kukaribisha Mathare North Youth.


Kariobangi inahitaji kushinda mechi moja ili kufikisha alama 100 na kufungia mahasimu wao Lucky Summer. Endapo itafanikiwa kushinda mechi hata Lucky Summer ikishinda mechi zote zilizosalia haitaweza kupiku Kariobangi.


Nayo Lucky Summer inayokamata nafasi ya pili imepangwa kualika Tumaini FC tayari kuendeleza mtindo wa kugawa gozi.''Tumeandaa vijana wetu tayari kushinda alama zote sita kuendelea kutembeza vipigo mbele ya wapinzani wetu,'' anasema kocha mkuu Kariobangi. Anaongeza kwamba ana imani tosha vijana watafanya kweli.


Kariobangi iliyoasisiwa mwaka uliyopita ikimaliza kileleni mwa kipute hicho itajikatia tiketi ya moja kwa moja kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa daraja ya pili muhula ujao. Kikosi hicho kinajivunia huduma za wachezaji mahiri kama Dennis Wafula, Bramuel Kavaya, Ian Onyango (nahodha), Prise Luvutse, Victor Kinyuli, George Karani, Tom Bonface na Lawrence Otieno.



Naye kocha wa Lucky Summer, Dan Nguya anasema wachezaji wake wanatosha mboga kuendeleza kasi yao na kunyamazisha Tumaini FC. ''Tunafahamu tuna kibarua kukabili wapinzani wetu maana nao pia wamejipanga kupigania ushindi wa pointi tatu,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kuwa hawana lingine bali wamepania kumaliza kati ya nafasi ya mbili bora ili kujikatia tiketi ya kujiweka pazuri kupanda ngazi wakipata nafasi.


Lucky Summer imekuwa kati ya wapinzani wakuu wa Kariobangi Legends tangia mwanzo wa michuano hiyo. Lucky Summer inategemea wachana nyavu wepesi kama Dennis Opiyo, Levis Odede, Rijkaard Otieno na Joel Arika kati ya wengine.


Naye kocha, Josiah Olang ataongoza Automech FC kuialika Rada Sports ugani Muthurwa. ''Bila shaka hakuna timu tunayodharau kwa hivyo tutakuwa makini zaidi tutakapokabili wapinzani wetu huku tukilenga kubeba alama tatu muhimu,'' anasema kocha wa Automech.


Anaongeza tayari ligi imeenda lakini lazima wapambane hadi mechi ya mwisho kusudi wamalize kati ya tano bora. Automech FC inategemea huduma za wachezaji shupavu kama Peter Wambua, Stephen Ajode. George Omondi na Musa Kombo.



Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, Tena United itachuana na Umoja Rhinos, Fortune Kinderen FC itaumana na Gor Mahia Youth, Soweto All Stars itamenyana na Ruai United huku Hakati Sportiff ikitifua vumbi dhidi ya Wendani Allstars. UEFA Despanol FC itakabili Gunners, Pumwani Sports itapepetana na Utawala Youth, Babadogo United itachuana na Santos huku Lula FC ikikutanishwa na Mathare North United.

 
 
bottom of page