Nane Zajipanga Kisa Moyo Bet Cup
- heartmediak4
- Oct 15, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 15 Oktoba 2024

TIMU nane zimethibitisha kushiriki shindano la makala ya kwanza kuwania taji la Moyo Bet Cup litakaoandaliwa uwanja wa Drive Inn Primary, Mathare Nairobi wikendi. Ngarambe hiyo imepangwa kung'oa nanga Jumamosi (tarehe 19 Oktoba) na kukamilika Jumatatu (tarehe 21 Oktoba) ambapo timu itakayoibuka bingwa itatuzwa Sh400,000. Orodha ya vikosi hivyo inajumuisha: FC Creative Hands iliyomaliza ya pili kwenye pambano la makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup.

Timu zingine zikiwa Mathare North Youth, Red Eagles, Mathare North United, Githurai All Stars, Mathare Flames, Kayole Masters na Kariobangi Legends Youth. ''Tuna imani na wachezaji wetu kwamba wana tosha mboga kufanya kweli na kutwaa ubingwa huo,'' alisema kocha wa Creative Hands, Samwel Kisolo. Aliongeza kuwa katika mpango mzima wamepania kujikaza kwa udi na uvumba kuhakisha wanaibuka kati ya nafasi tatu bora ili kutia mfukoni tuzo ya Sh150,000. Timu itakayomaliza nafasi ya pili itapongezwa kwa Sh250,000. Creative Hands iliibuka ya pili kwenye michuano ya Ruben FM Cup ilipozabwa kwa mabao 5-4 na Wilson Aviators FC kwa mipigo ya matuta baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika muda wa kawaida.
Naye mwenyekiti wa Kariobangi Legends Youth, Eric Atanga Otieno anajipiga kifua kuwa wachezaji wake wana uwezo wa kutetemesha wapinzani wao na kutawazwa mabingwa wa kipute hicho. ''Bila kujipigia debe ninaamini wachezaji wangu watafanya vizuri kwenye michuano hiyo na kumaliza kidedea,'' alisema mwenyekiti huyo. Alitoa wito kwa vijana wake kuwa makini kujituma bila kuhofia wapinzani wao maana wadhamini wanatoa tuzo nzuri.
Kariobangi inayoshiriki mechi za Kundi C kuwania taji la Ligi ya Taifa Daraja la Pili inajivunia wachana nyavu kama Bramuel Kavaya, Robbie Maangi, Paul Okumu, Victor Kinyili, Idris Amadi na Laurence Otieno kati ya wengine.


