Mwenyekiti wa K.L. Y Amepongeza Vijana wake huku Saba Wakitimuliwa
- heartmediak4
- Sep 17, 2024
- 1 min read
Na HERAT MEDIA
Jumanne, 17 Septemba 2024
MWENYEKITI wa Kariobangi Legends Youth (K.L.Y), Eric Atanga Otieno amepongeza vijana wake kwa kunasa tiketi ya kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu mpya. ''Bila shaka tunafuraha na tunashukuru Mola baada ya vijana wetu kufanya kazi nzuri ndani ya msimu uliyopita na kutimiza azma yetu,'' anasema. Anaongeza kuwa haikuwa mteremko kwani walikabili milima na mabonde lakini hatimaye kufanya kweli.

Kariobangi Legends Youth iliyokuwa inashiriki mechi za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) ilimaliza kidedea kwa kuzoa alama 110, sita mbele ya mahasimu wakuu Lucky Summer. Kariobangi chini ya nahodha, Ian Onyango ilishinda mechi 35, kutoka nguvu sawa mara tano kisha kupoteza patashika mbili. Kariobangi ndio iiliyopoteza mechi chache kabisa maana iliyoifuata ilikuwa Lucky Summer iliyopoteza mechi sita huku timu zingine zikipoteza kuanzia patashika kumi. Mwenyekiti huyo anashikilia kwamba wamepania kuendeleza ubabe wao kwenye mechi za ligi mpya. Anadokeza kuwa wamepania kutimiza mipango wa kila mwaka kushiriki daraja moja na kusonga mbele.

''Kama kawaida tunalenga kushiriki msimu mmoja katika daraja la pili na kubeba tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki daraja la kwanza,'' akasema.
Kwenye juhudi za kusuka kikosi hicho, Kariobangi Legends Youth imetimua wachezaji saba pia aliyekuwa kocha wake mkuu, Geoffrey Wangalwa.
Kocha huyo akiongea na Heart Media Dijitali alisema anatakia wachezaji wa klabu hiyo na menejimenti yake kila la heri.
Orodha ya wachezaji ambao wameonyeshwa mlango inashirikisha:Moving Omondi. Peter Kepher, Milton Ouma, Michael Okoth, Yusuf Baboya, Eugene Mutava na Tom Bonface. Tayari uongozi wa klabu hiyo umetambua pia umeanza majadiliano na wachezaji wanaopania kujaza nafasi za waliotimuliwa.



