Mpango Mzima Huu Hapa Nusu Fainali Gozi la Koth Biro
- heartmediak4
- Nov 24, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumapili 24, Novemba 2024

KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa kwenye nusu fainali za makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro zitakaochezewa uwanjani Umeme Ziwani, Nairobi. Mechi hizo zimepangwa kuchezwa Jumatatu hii tarehe 25, Novemba 2024. Mbuta FC itashuka dimbani kukabili Kiambiu Warriors FC nayo Watch and Learn FC itaingia mzigoni kuchuana na Mathare Commban FC.
''Bila shaka tumeandaa vijana wetu vizuri kukabili wapinzani wetu ambapo dhamira kuu itakuwa kubeba ushindi ili tujitose katika fainali ya mwaka huu,'' anasema kocha wa Watch and Learn, Abdimajid 'Naja' Mumin. Anangeza kwamba wanafahamu Mathare Commban FC imepania kuvuruga mpango wao. Aidha anadokeza kuwa ni mara ya kwanza timu yenye hasili ya kisomali kufuzu kwa nusu fainali za koth biro. Pia anashikilia kwamba huenda wakaibuka mabingwa wa kipute cha mwaka huu. Watch and Learn FC inajivunia huduma za wachezaji kama Ahmed Abdi, Douglas Nyaosi na Morris Oduor kati ya wengine.

Naye kocha wa Mbuta FC, Caleb Osodo alisema kamwe hawawezi kudharau wapinzani lakini hawatakuwa na lingine mbali lazima wapambane mwanzo mwisho kwenye mechi hiyo. ''Kawaida tumepania kushiriki mechi hiyo kama michuano iliyopita tukilenga kunasa tikiti ya kusonga mbele kushiriki fainali ya mwaka huu,'' anasema kocha huyo. Aliongeza kuwa kamwe hawana hofu dhidi ya wapinzani wao.

Kwenye robo fainali, Watch and Learn ilikung'uta Kayole Select FC kwa mabao 3-1. Nayo Mbuta FC ilinyuka Kamkunji FC bao 1-0, Mathare Commban ilishinda Pumwani Sports Club iliyokuwa bingwa mtetezi kwa mabao 2-1 huku Kiambiu Warriors ikibeba ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Kariadudu FC. Watch and Learn FC inajivunia kutwaa taji la The Rissa Football Tournament kwenye mechi zilizofanyika Jumamosi tarehe 8, Septemba 2024 ugani Nairobi Sailing Club, Lang'ata Nairobi. Katika fainali Watch and Learn iliangusha Tabiban FC kwa mabao 4-2 katika fainali baada ya kurarua Villaroma FC kwa mabao 5-1 kwenye nusu fainali.


