top of page
Search

Mozzartbet Yaipiga Jeki Malkia Strikers kwa Sh2 milioni

  • heartmediak4
  • Jun 26, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumatano, 26 Juni 2024

TIMU ya Voliboli ya wanawake maarufu Malkia Strikers imepigwa jeki baada ya kupokea Sh2 milioni kutoka kwa Shirika la kubeti la Mozzartbet. Vipusa hao wanaojiandaa kushiriki ngarambe ya Challenger Cup nchini Ufilipino na Michezo ya Olimpiki 2024 Paris, Ufaransa walikabidhiwa hundi ya fedha hizo Jumanne tarehe 25 Juni kwenye hafla iliyoandaliwa Kasarani Stadium, Nairobi



Mwaka uliyopita Shirika hilo lilitia saini mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kitita cha 15 milioni. ''Sh2 milioni zitaendea wachezaji na kamati ya kikosi hicho pekee ili kuwatia motisha kwa mashindano yajayo,'' alisema mwenyekiti wa Shirikisho la Voliboli ya Kenya (KVF), Charles Nyaberi. Alishukuru Mozzartbet kwa kuendelea kusapoti Malkia Strikers. Kwa jumla alishukuru wafadhili wote ikiwamo Wizara ya Michezo, Kituo cha Kukuza Talanta cha Kenya na Java House.



Alidokeza kuwa katika Olimpiki wanalenga kufanya vizuri kuliko kwenye makala ya 2020 walipobanduliwa katika makundi ili waimarishe msimamo wao duniani.


Afisa Mkuu wa Mozzartbet, Sasa Krneta alisifia Malkia Strikers kwa kufanya vizuri katika mchezo huo barani Afrika. ''Tutazidi kurefusha mkataba wetu na Malkia Strikers kwenye juhudi za kuipiga jeki ili kufanya vizuri kimataifa,'' alisema. Aliongeza kuwa wakifanya vizuri kwenye mashindano yajayo bila shaka watawatuza vinono. Alisisitiza kuwa wataendelea kufadhili michezo tofauti hapa nchini.



Kocha wa Malkia Strikers, Japheth Munala alisema wapo tayari kwa mashindano hayo mawili yajayo wanakolenga kutumia Challenger Cup kupima uwezo wa kikosi hicho. ''Nilitamani sana kushiriki Olimpiki ambapo azma yangu imetimia nitaongoza wezangu kwenye makala ya mwaka huu,'' alisema nahodha, Trizah Atuka. Alishukuru Mozzartbet kwa kuendelea kuwashika mkono kwenye juhudi za kupeperusha bendera ya Kenya kimataifa. Alidokeza kuwa wamepania kujituma kiume angalau washinde mechi moja.


Malkia Strikers itashiriki Challenger Cup itakayofanyika Julai 4 hadi 7 nchini Ufilipino. Mechi hizo zitajumuisha: Argentina, Jamhuri ya Czech, Kenya, Vietnam, Ubelgiji, Uswidi, Puerto Rico na wenyeji Ufilipino. Kisha itaelekea jijini Miramar, Ureno kwa mazoezi ya mwisho inakotazamiwa kushiriki mechi nne za kirafiki dhidi ya timu za mataifa mengine vile vile baadhi ya vikosi vya wenyeji. Baadaye itaelekea jijini Ufaransa kwa Olimpiki ambapo imepangwa Kundi B.

Kundi hilo linajumuisha: mabingwa watetezi Brazil na Polland ambazo pia zimepangwa nafasi ya kwanza na nne kwenye viwango vya mchezo huo duniani (FIVB) pia Japan.

 
 
bottom of page