top of page
Search

Midume wa Kenya Waibuka 10 Kombe la Dunia Hoki ya Masters

  • heartmediak4
  • Oct 25, 2024
  • 2 min read

Na HERAT MEDIA

Ijumaa, 25 Oktoba 2024



TIMU ya taifa ya wanaume kwa waliozidi umri wa miaka 40 ilimaliza nafasi ya kumi kwenye shindano la Kombe la Dunia la hoki ya Masters lililoandaliwa jijini Cape Town, Afrika Kusini. Ilikuwa mara ya kwanza Kenya kushiriki pambano hilo.

Mechi ya mwisho Kenya ya kocha, Meshack Senge ilitoka nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya Argentina baada ya kuzabwa mabao 2-1 na Marekani kwenye nusu fainali ya kuwania nafasi ya tisa.

Kando na matokeo hayo Kenya iliyokuwa imepangwa Kundi C ilibeba ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Singapore pia ilitoka sare tasa na Alliance International Masters Community (All IMC). Kisha ilizabwa mabao 2-1 na Malaysia pia ilikung'utwa magoli 6-2 na Ujerumani.




''Bila shaka ulikuwa ufanisi mkubwa kwetu licha ya kutofanya vizuri kwenye ngarambe hiyo,'' anasema meneja wa kikosi hicho, Moses Majiwa. Anashukuru wafadhili wote waliofanikisha ndoto ya kikosi hicho kushiriki pambano hilo. Anashikilia kwamba wanatarajia kufanya vizuri kwenye mashindano ya miaka ijayo. Kadhalika anatoa wito kwa wachezaji zaidi kujiunga na kikosi hicho kukipiga jeki.

Kenya iliibuka ya kumi mbele ya Marekani kati ya vikosi vilivyotetemesha kwenye kipute hicho. Katika mechi za makundi ilimaliza ya nne kwa alama nne. Nayo Ujerumani iliyoshinda mechi zote iliibuka kidedea kwa alama 12, sita mbele ya Malaysia sawa na Singapore tofauti ikiwa idadi ya mabao. Alliance International Masters Community (ALL IMC) ilimaliza ya tano kwa alama moja.


Kando na kitengo cha waliozidi miaka 40 kwa wanaume na wanawake shindano hilo limevutia timu za wanaume waliozidi umri wa miaka 65, 70 na 75. Timu ya Kenya inajumuisha wachezaji kama: Ajay Dosaja, Michael Obuya, Eli Asura, Farhan Khan, Samuel Oungo, Joab Ondiro, Arif Shah (nahodha), Bill Olang, Harpreet Seehra, Friday Mathews na Amritpal Ghataurhae. Wengine ni Asif Shah, Willis Okeyo, Barnabus Odhiambo, Aseem Joshi, Wycliffe Ongori, Inderjit Matharu, Parraj Sehmi, Kennedy Kyalo na Herminder Singh. Safari ya timu hiyo ilifadhaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Kenya Airways, Daikyo Japan Motors, Meximed International (K) Limited, ACK Autopix, Trade Routes, Sikh Union Club, Dime Credit, Filmline Limited na Interor Inspirations Limiited.

 
 
bottom of page