top of page
Search

Mfahamu Kocha Anayewapa Mzuka Vijana wa Kariobangi Legends Youth

  • heartmediak4
  • Jul 15, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumatatu, 15 Julai 2024


INGAWA ananoa klabu ya viwango vya chini, Geoffrey Wangalwa ni kati ya makocha wanaopania kutinga upeo wa juu katika taaluma hiyo. Katika mpango mzima analenga kuwa kocha wa kiwango cha CAF B kwani tayari amehitimu kwa viwango vya C na D. Wangalwa aliyeanza ukufunzi mwaka 2018 akichezea Kariobangi Sharks ya Ligi Kuu ya FKF-PL ndiye kocha wa klabu mpya ya Kariobangi Legends Youth.

Klabu hiyo iliasisiwa mwaka uliyopita (2013) ambapo ni kati ya vikosi vinavyotetemesha sio haba kwenye kampeni za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi (NERL) msimu huu.



''Mwanzo wa ngoma nikiwa mchezaji wa Kariobangi Sharks nilikuwa nafunza wachezaji wa klabu hiyo wasiozidi umri wa miaka 12 maana napenda kutumia kipaji changu kusaidia wengine,'' anasema. Anaongeza kwamba jeraha la mguu lilimsukuma zaidi kujitosa katika ukufunzi.

Wangalwa anajivunia kuchezea Kariobangi Sharks, Mathare North Youth na Nairobi Stima. ''Nilipigia Kariobangi Sharks ikishiriki Supa Ligi (NSL) kabla ya kuitema na kujiunga na Nairobi Stima,'' akasema. Alisakatia Mathare North Youth kwa misimu miwili kisha mwaka 2013 alirejea Kariobangi Sharks ilipopata ufadhili. Aliichezea kwa mihula miwili na kuwa kati ya wachezaji walioisaidia kupandishwa ngazi kushiriki ligi kuu. Bosi wa Kariobangi Sharks, Nick Mwendwa ambaye ndiye rais wa FKF alifurahi zaidi alipogundua Wangalwa alikuwa kocha mwenye bidii.



Hata hivyo tatizo la mguu lilimfanya kuacha kucheza lakini alisalia kuwa kati ya manaibu wa kocha wa klabu hiyo, William Mluhya.

Vile vile alikuwa akinoa kikosi cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 12, miaka 14 na miaka 17. Anajivunia kunoa makucha ya wachezaji kadhaa ambao kwa sasa wanashiriki ligi kuu akiwamo Geoffrey Onyango na Isack Wasambo wa Kariobangi Sharks..

Kama tujuavyo, mtoto akikua hutoka katika boma ya wazazi wake ili kuanzisha boma lake. Mwaka 2022, Wangalwa aliamua kuitema Kariobangi Sharks ambapo alipata ajira ya kunoa akademia ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18 ya Vision Soccer ambayo hupatikana mtaani Karen, Nairobi. Baadaye mapema mwaka 2023 alikutana na mwasisi wa Kariobangi Legends Youth, Eric Atanga ambapo baada ya kupiga soga waliwazia kubuni kikosi hicho.



Kwa sasa kocha huyo anashirikiana na Jeremiah Khayo kunoa Kariobangi Legends Youth ambayo hadi sasa inaongoza katika msimamo wa kipute hicho kwa kuzoa alama 73, sita mbele ya Lucky Summer FC baada ya kushiriki mechi 29 na 31 mtawalia.

Anasema kuwa wamepania kuhakikisha wanashiriki ngarambe hiyo kwa msimu mmoja na kuzoa tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya Pili muhula ujao. Anashikilia kuwa vijana wake wanajituma kwa udi na uvumba kwenye kipute hicho kinaoshusha ushindani wa kufa mtu. Wangalwa alitua duniani mwaka 1992, alisomea Shule ya Msingi ya Daniel Komboni, Kariobangi North Nairobi kisha alisomea Shule ya Upili ya Anoitted.

 
 
bottom of page