top of page
Search

Mechi za Nusu Fainali za Ruben FM Cup Kupigwa Jumapili hii

  • heartmediak4
  • Sep 27, 2024
  • 1 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 27 Septemba 2024



MECHI za nusu fainali za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup zitachezwa Jumapili hii tarehe 29 Septemba 2024 ugani Vision Mukuru Kwa Njenga Embakasi, Nairobi. Timu moja kati ya mbili ambazo ndio mara ya kwanza kushiriki ngarambe hiyo lazima ibandubiliwe pale Wilson Aviators itakapokutanishwa na Meteorite FC. Kwenye nusu fainali ya pili, Ruben United itakabili Creative Hands.

''Kama kawaida tumepania kujituma kwa udi na uvumba kukabili wapinzani wetu wala hatuwezi kuwadharau maana walipigana kiume ili kufuzu kwa nusu fainali,'' anasema kocha wa Meteorite, Catherine Muoka, Anaongeza kuwa ana imani watafanya kweli mbele ya wapinzani wao na kutinga katika fainali. Aidha anadokeza kuwa itakuwa furaha kwao kushiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza na kutawazwa mabingwa. Kwenye mechi za robo fainali, Meteorite ilipiga Mukuru Wazee kwa mabao 5-3 kupitia penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1. Meteorite inajivunia huduma za wachezaji mahiri kama Philip Omasaja na Sylvester Patrick kati ya wengine.


Nayo Wilson Aviators ilitinga nusu fainali iliponyamazisha Kamongo FC kwa mabao 4-3 kupitia mipigo ya penalti baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida. Wilson Aviators itategemea wachezaji shupavu kama Reyvans Kinesi, Hanington Kahi, Allan Chekaya, Sylvester Lichama (nahodha) na Brian Mwania.

Kwenye robo fainali, Creative Hands ilibeba bao 1-0 mbele ya Young Warriors. Nayo Ruben United ilikomoa Vision FC kwa mabao 4-3 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1.

Mshindi wa kitengo cha wanaume mwaka huu atatuzwa Sh100,000. Timu itakayoibuka nafasi ya pili itapokea Sh70,000 kisha nafasi ya tatu na nne zitapongezwa kwa Sh40,000 na Sh20,000 mtawalia.



 
 
bottom of page