Mechi Za NERL Kukunja Jamvi Wikendi Hii, Huku Kariobangi Legends Youth Ikijivunia Kumaliza Kibabe
- heartmediak4
- Aug 30, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa, 30 Agosti 2024
KAMPENI za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NWRL) zitakamilika wikendi hii, baada ya Kariobangi Legeds Youth kumaliza kibabe kwenye mechi za Jumatano tarehe 28 Agosti. Kariobangi Legends Youth ambayo tayari imetwaa ubingwa wa taji hilo ilipepeta Mathare North United kwa mabao 4-0 na kumaliza kampeni zake kiume. Magoli hayo yalipatikana kupitia juhudi zake Victor Kinyuli, Ian Onyango, Dennis Wafula na Bramwel Kavaya.
''Tunamshukuru Mola kwa kutusaidia kuhakikisha tumemaliza mechi zetu kwa ushindi mnono ingawa tulimaliza kibarua chetu mapema,'' anasema kocha wa Kariobangi, Geoffrey Wangalwa. Anaongeza kuwa sasa wanajiandalia kibarua kijacho hasa kutafuta bingwa wa kipute hicho. Kwenye ratiba ya kipute hicho Jumamosi hii tarehe 31 Agosti, kocha Dan Nguya ataongoza Lucky Summer kukabili Gunners ugani Embakasi Garisson, Embakasi.

''Bila shaka hata tukishinda mechi yetu hakuna tofauti itakayokuwepo isipokuwa kuongezea alama tatu na mabao lakini bado tutaibuka nafasi ya pili,'' anasema kocha wa Lucky Summer. Hata hivyo anaongeza kuwa wangependa sana kumaliza kwa kutia kapuni ushindi mkubwa mbele ya wapinzani wao.
Anashikilia ana imani wachana nyavu wake wanatosha mboga kutetemesha wapinzani wao na kutimiza azma ya kusajili pointi tatu muhimu na mengine kumuachia Mungu.
Utawala Youth na Babadogo United kila moja itakuwa mbioni kuwinda pointi tatu muhimu ili kuiwezeha kumaliza kati ya nafasi tatu bora kwa kuzingatia kwa sasa zimevuna alama 81 kila moja. Utawala Youth ya kocha, Bill Oporia itaingia mzingoni kuchuana na Wendani Allstars inayofuta mkia katika jedwali.
''Tumeshiriki mazoezi ya kutosha tukijiandalia mechi ya mwisho kwani tumepania kujituma kiume angalau kubeba ufanisi wa pointi tatu na kumaliza kati ya nafasi tatu bora,'' anasema kocha wa Utawala Youth.

Anaongeza kuwa tayari wamelemewa kubeba tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya Pili lakini bado watakuwa wakinusa njia zote wakibahatika wapite nayo.
Nao wanasoka wa Babadogo United watakuwa ugenini kuchuana na Mathare North Youth ambapo lazima wawe makini zaidi dhidi ya wenyeji hao. ''Tumepania kupambana kiume kuhakikisha tumevuna alama tatu muhimu tena kwa ushindi wa mabao mengine tuone kama tuwapiku wapinzani wetu,'' anasema meneja wa Babadogo, Ben Wanjala. Anaongeza kuwa wana kibarua kigumu kwenye mchezo huo kwa kuzingatia Mathare North Youth huwa inachanganya wapinzani wao.

Kwenye michuano hiyo, Automech FC itamenyana na Hakati Sportiff, Gor Mahia Youth itacheza na Tena United, Ruai United itakabili Umoja Rhinos, Rada itatifua vumbi dhidi ya Fortune Kinderen huku Tumaini FC ikicharazana na Soweto All Stars. Nao vijana wa Lula FC watapepetana na Pumwani Sports Club huku Santos Hotspurs ikikutanishwa na UEFA Despanol FC.


