Mathare Flames, Mathare Queens Mabingwa Eastlando Moyo Bet Cup
- heartmediak4
- Oct 23, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumatano, 23 Oktoba 2024
TIMU ya wanaume ya Mathare Flames na kina dada wa Mathare Queens zimeonyesha ubabe wazo na kutwaa taji la makala ya kwanza ya Eastlando Moyo Bet Cup kwenye mechi zilizochezewa (Jumatatu 21, Oktoba 2024) ugani Drive-inn, Mathare North Nairobi. Katika Mathare Flames ilidunga majira zao Mathare North United kwa bao 1-0. .
Kwa wanawake, Mathare Queens ya kocha, Maxwell Efedha ilibeba ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kariobangi Sharks. Mathare Flames ilituzwa Sh300,000 nayo Mathare North United ilipokea Sh200,000. Upande wa Mathare Queens ilitia kapuni Sh200,000 huku Kariobangi Sharks ikipongezwa kwa Sh100,000.

Katika fainali ya wanaume timu zote zilionyesha mechi safi ambapo kipindi cha kwanza kiliisha zikiwa sare tasa. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku vijana wa Mathare Flames wakionekana kufufua mchezo wao. Mathare Flames ilipata bao hilo la pekee kupitia juhudi zake Morris Mutua. ''Hiyo mechi haikuwa mteremko maana wachezaji wote wanafahamiana lakini vijana wangu walipata nafasi moja na kuitumia ipasavyo pia kutimiza azma yetu,'' alisema kocha wa Mathare Flames. Alishukuru waandalizi wa kipute hicho akitaja kuwa mechi hizo zilitoa nafasi nzuri kwa wachezaji walioshiriki kuonyesha talanta zao.

Mwakilishi wa shirika la Moyo Bet, Jackson 'Miheso' Mitalo alisema huo ni mwanzo tu bali wamepania kuendelea kuandaa mashindano sawia na hayo siku zijazo.
''Ninashukuru timu zote zilizoshiriki shindano la makala ya kwanza kwani wachezaji husika walitoa burudani tosha kwa wapenzi wa mchezo wa kabumbu,'' alisema. Aliongeza kuwa shirika hilo hujihusisha na mambo mengi kusaidia wananchi ikiwamo hospitali, Shule, Mayatima na wasiojiweza.
Kwa wanaume Githurai All Stars (GAS) ya kocha, Fredrick Ochieng ilimaliza ya tatu kwa kuzoa mabao 3-1 dhidi ya Mathare Masters. GAS ilipata mabao hayo kupitia Moise Kurureza aliyecheka na wavu mara mbili naye Erick Kuria alitikisa wavu mara moja. GAS ilituzwa SH100,000 huku Mathare Flames ikipongezwa kwa Sh75,000.
Kwenye nusu fainali, Mathare Flames iligonga Kayole Masters kwa magoli 4-1 nayo Mathare North United ilibeba mabao 2-1 mbele ya GAS. Kitengo cha wanawake, Kariobangi Sharks ilichapa Kariobangi Sports kwa mabao 5-3 kupitia mipigo ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1.Nayo Mathare Queens iliangusha Mathare North kwa mabao 4-0.

Kwenye robo fainali za wanaume, Mathare Flames ilichapa Kariobangi Legends Youth bao 1-0, Mathare North Youth ilipigwa mabao 4-2 na GAS kupitia penalti baada ya kutoka mabao 2-2. Mathare North United ilibeba bao 1-0 mbele ya FC Creative Hands huku Kayole Masters ilicharaza Red Eagle kwa mabao 3-1.


