top of page
Search

Masters Hockey: Kenya Kufungua Ngarambe ya Kombe la Dunia Dhidi ya Malaysia

  • heartmediak4
  • Oct 11, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 11 Oktoba 2024


MICHUANO ya magongo ya Masters kuwania taji la Kombe la Dunia kitengo cha wanaume na wanawake kwa viwango tofauti imeratibiwa kukunjua jamvi Jumamosi hii tarehe 12, Oktoba jijini Cape Town, Afrika Kusini. Ngarambe hiyo imepangwa kukamilika Oktoba 21.

Timu ya wanaume ya Kenya kwa waliozidi umri wa miaka 40 imepangwa kuingia mzigoni Jumamosi hii kukabili Malaysia kwenye mechi za Kundi C kitengo hicho. Timu ya Kenya inayoshiriki ngarambe hiyo kwa mara ya kwanza imepania kujituma kiume kwenye mechi hizo.


Kocha wake, Meshack Senge anashikilia kuwa kamwe hawana fresha bali wamepania kuonyesha jinsi wanaweza. ''Jambo la kwanza hatujawahi kushiriki mechi za kiwango hicho pia hatujawahi kucheza dhidi ya wapinzani wetu,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kuwa nyumbani hawakuwa wakishiriki mechi zenye ushindani mkubwa maana hawajawahi kucheza na mataifa mengine. Wachezaji wa kikosi wamekuwa wakishiriki mechi za michuano ya masters Series pia migarazano ya kupimana nguvu.

Kwa wanaume waliozidi miaka 40 shindano hilo litajumuisha timu 14 ambazo zimegawanywa katika makundi matatu. Kenya imepangwa Kundi C linaloshirikisha Ujerumani, Malaysia, Singapore na All International Masters Community (ALL IMC). Kundi A lina:Uingereza, Amerika, Afrika Kusini na Australia International Masters Community. Nalo Kundi B linajumuisha: Australia, Ufaransa, Argentina, New Zealand na Afrika Kusini International Masters Community.



Timu ya Kenya inashirikisha wachezaji kama:Ajay Dosaja, Michael Obuya, Eli Asura, Farhan Khan, Samuel Oungo, Joab Ondiro, Arif Shah (nahodha), Bill Olang, Harpreet Seehra, Friday Mathews na Amritpal Ghataurhae. Wengine ni Asif Shah, Willis Okeyo, Barnabus Odhiambo, Aseem Joshi, Wycliffe Ongori, Inderjit Matharu, Parraj Sehmi, Kennedy Kyalo na Herminder Singh.

Maofisa wao: Meshack Senge (kocha), Moses Majiwa, John Fernades, Del Mudher na Ashish Sharma (daktari).

Safari ya kikosi hicho ilifadhaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Kenya Airways, Daikyo Japan Motors, Meximed International (K) Limited, ACK Autopix, Trade Routes, Sikh Union Club, Dime Credit, Filmline Limited na Interor Inspirations Limited.

 
 
bottom of page