top of page
Search

Mapambano Makali Kushuhudiwa Kwenye Mechi za NERL

  • heartmediak4
  • Jul 19, 2024
  • 2 min read

Na HEAR MEDIA

Ijumaa, 19 Julai 2024

MAPAMBANO makali yanatazamiwa kushuhudiwa wikendi hii kwenye kampeni za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL). Jumamosi hii tarehe 20 Julai, vinara wa kipute hicho, Kariobangi Legends Youth itakuwa ugenini kukabili Maafande wa Gunners ugani Garison, Embakasi kwenye patashika iliyopigiwa chapuo kuzua ushindani mkali. Kisha Jumapili tarehe 21 Julai, Kariobangi itakuwa katika ardhi ya kiamboni, Kariobangi North Primary kukaribisha wageni wao Soweto All Stars.



Kwenye patashika nyingine ya Jumapili tarehe 21 Julai, mahasimu wakuu Lucky Summer FC imepangwa kucheza na majirani zao Babadogo United ugani Babadogo. ''Tumeandaa wachezaji wetu imara tayari kukabili wapinzani wetu lengo kuu likiwa kuzoa alama zote muhimu na kujiongezea tumaini la kuwapiku wapinzani wetu,'' anasema kocha wa Lucky Summer, Dan Nguya. Anaongeza kuwa lazima wajitume kiume maana ushindi wa mechi hiyo utakuwa muhimu zaidi kwenye kampeni zao kufukuzia tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu ujao. Aidha anashikilia kuwa endapo wataendeleza mtindo wa kushinda mechi zijazo wakilemewa kutwaa taji hilo watajiweka pazuri kumaliza kati ya nafasi mbili bora na kuzoa tiketi ya kusonga mbele. Lucky Summer inajivunia huduma za wachezaji hodari kama Dennis Opiyo, Levis Odede, Rijkaard Otieno na Joel Arika kati ya wengine.

Meneja wa Babadogo, Ben Wanjala anadokeza kuwa vijana wake wamo tayari kukabili wapinzani wao. ''Hakika wageni wetu wasitarajie mteremko bali wafahamu kuwa tumejipanga kiume kuwakabili,'' anasema. Anaongeza kuwa ushindi wa mechi hiyo utawapiga jeki pakubwa kwenye kampeni zao.



Naye kocha wa Kariobangi, Geoffrey Wangalwa anasema kuwa wanafahamu wapinzani wao wamejipanga kuwavuruga lakini wamejipanga kushusha soka la kibiashara. ''Ninachofahamu lazima tuwe makini zaidi mbele ya wapinzani wetu lengo kuu likiwa kuwazima na kubeba alama zote muhimu,'' anasema. Anaongeza kuwa kamwe hawataki kulaza damu dimbani maana wamegundua wakiteleza tu watakuta mwana sio wao. Kariobangi Legends Youth inategemea huduma za wachezaji wepesi kama Victor Kinyuli, Bramwel Kasaya, George Karani, Ian Onyango (nahodha), Tom Bonface na Lawrence Otieno Kati ya wengine.

Kwenye mfululizo wa kipute hicho, Jumamosi hii Pumwani Sports Club itakaribisha Wendani All Stars, Mathare North Youth itamenyana na Fortune Kinderen, Hakati Sportiff itaumana na Tumaini FC huku Lula FC ikichuana na Umoja Rhinos.


Jumapili Gunners ya kocha, Brian Kaka kwa mara nyingine itakuwa nyumbani kuialika Rada Sports, kocha Bill Oporia ataongoza Utawala Youth kukaribisha Ruai United ugani Kinkar. Automech FC itazuru ugani Drive-Inn kucheza na Mathare North United, Tena United itapepetana na UEFA Despanol nayo Santos Hotspurs itakutanishwa na Gor Mahia Youth.

Kwenye msimamo wa ngarambe hiyo, Kariobangi Legends Youth ingali kifua mbele kwa kuzoa alama 73, sita mbele ya Lucky Summers baada ya kuingia mzigoni mara 29 na 31 mtawalia. Babadogo United inashikilia tatu bora kwa alama 64, moja mbele ya Utawala Youth.





 
 
bottom of page