top of page
Search

Malkia Strikers Wazima Salon de Provence Japo Kirafiki

  • heartmediak4
  • Jul 24, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumatano, 24 Julai 2024




TIMU ya voliboli ya wanawake maarufu Malkia Strikers iliangusha wenyeji Salon De Provence kwa seti 3-0 kwenye mechi ya kirafiki iliyochezewa jijini Miramas, Ufaransa. Warembo hao chini ya nahodha Trizah Atuka na Edith Wisa walivuna ushindi wa alama 25-14, 25-14, 25-14. Ulikuwa ushindi wa pili baada ya kubeba seti 3-0 dhidi ya Istres Provence.

Wasichana hao wapo nchini Ufaransa kushiriki makala ya mwaka huu ya Michezo ya Olimpiki. ''Sina shaka kutaja kuwa kwenye mechi hizo mbili warembo walionyesha mechi nzuri na kuashiria wanaimarisha mchezo wao,'' alisema kocha mkuu, Japheth Munala. . Aliongeza kuwa kwenye kampeni hizo watakuwa mbioni kuwinda angalau ushindi mmoja licha ya kwamba wanatarajia ushindani mkali.


Malkia Strikers inayoshirikisha wachezaji 13 inapigwa jeki na wana dada wawili ambao hushiriki voliboli ya kulipwa katika mataifa ya bara Ulaya. Wawili hao ni

Sharon Chepchumba ambaye huchezea PAOK aliyojiunga nayo akitokea klabu ya Aris Thessaloniki. Mwingine ni Veronica Adhiambo ambaye hupigia Tarsus Belediyespor ya Uturuki.

Kwenye ngarambe hiyo Kenya imepangwa Kundi B linalojumuisha: mabingwa watetezi Brazil, Japan na Poland. Katika msimamo wa viwango vya mchezo huo duniani (FIVB), Brazil inakamata nafasi ya pili. Polland na Japan zinashikilia nafasi ya nne na saba mtawalia ilhali Kenya inafunga 20 bora.


Itakuwa mara ya nne kwa Malkia Strikers kushiriki Michezo ya Olimpiki baada ya kucheza mwaka 2000 (Sydney, Australia), mwaka 2005 (Athens, Ugiriki) na mwaka 2020 (Tokyo, Japan). Hata hivyo baada ya kushiriki makala ya mwaka 2005 ilikosekana kwa miaka 16 ambapo haikushiriki makala ya mwaka 2008 (Uchina), mwaka 2012 (Uingereza) na 2016 (Brazil).


Kikosi kamili: Agripina Kundu, Sharon Chepchumba, Loice Simiyu, Pamela Adhiambo, Veronica Adhiambo, Juliana Namutira, Leonida Kasaya, Trizah Atuka (nahodha) na naibu wake Edith Wisa. Wengine Emmaculate Nekesa, Belinda Barasa, Lorine Chebet na Esther Mutinda.

Maofisa: Ofisa wa kiufundi, Paul Bitok, makocha Japheth Munala na Josp Barasa, kocha wa kupiga tizi, Janet Wanja na Mududa Waweru(daktari).

 
 
bottom of page