Malkia Strikers Kusaka Ushindi wa Kwanza dhidi ya Japan Voliboli ya Olimpiki
- heartmediak4
- Aug 3, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa, 02 Agosti 2024

VIPUSA wa Malkia Strikers Jumamosi hii ya tarehe 3 Agosti wataingia dimbani kukabili Japan kwenye mechi ya mwisho Kundi B katika voliboli ya Michezo ya Olimpiki inayoendelea jijini Paris, Ufaransa. Malkia Strikers ya makocha, Japheth Munala na James Barasa watashiriki mechi hiyo huku wakiumiza majeraha ya kuangukia pua mara mbili kwa kukubali kichapo cha seti 3-0 mikononi mwa Brazil na Poland.
Warembo hao wakiongozwa na nahodha, Trizah Atuka wangali mbioni kuwinda angalau ushindi wa seti moja kwenye michuano hiyo wanaoshiriki kwa mara ya nne. Malkia wamepangwa Kundi hilo linaloshirikisha timu ambazo zipo mbele yao kwenye viwango vya mchezo huo duniani.
Katika viwango hivyo, Brazil inashikilia nafasi ya pili, Poland ya nne nayo Japan imekamata nafasi ya saba huku Kenya ikitua nafasi ya 20 ikiwa ndio inaongoza barani Afrika.
''Bado hatujavunjika moyo tunajiamini tunaweza kutimiza azma yetu kwenye mchezo huo,'' alisema nahodha huyo. Aliongeza kuwa hali imekuwa balaa kwao hasa baada ya kukosa ujanja kwenye mechi zilizopita. Kinaya Malkia ilishindwa kwenye mechi hizo kila moja chini ya dakika 60.
Katika msimamo wa mechi za Kundi hilo, Brazil inaongoza kwa alama sita sawa na Poland tofauti ikiwa idadi ya seti za ushindi baada ya kila moja kuzamisha Japan na Kenya. Japan inashikilia nafasi ya nne bila alama yoyote sawa na Kenya. Japan imeipiku Kenya maana ilishindwa na Poland kwa seti 3-1 ilhali Kenya haijapata seti yoyote kwenye mechi zote mbili ilizoshiriki. Kwenye makala ya mwaka 2020 jijini Tokyo, Japan Malkia Strikers walishindwa kufana na kumaliza nafasi ya 12.


