top of page
Search

MAGONGOWanaume wa Magongo ya Masters Wamo Afrika Kusini Kushiriki Kombe la Dunia

  • heartmediak4
  • Oct 9, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumatano, 9 Oktoba 2024




TIMU ya taifa ya wanaume ya magongo ya Masters kwa waliozidi umri wa miaka 40 jana jioni ilitua jijini Cape Town, Afrika Kusini tayari kushiriki fainali za Kombe la Dunia. Mechi za ngarambe hiyo zitaandaliwa Oktoba 12-21 mwaka huu na ndio mara ya kwanza Kenya kushiriki kidumbwedumwe hicho. ''Ndio mara ya kwanza wala hatufahamu kiwango cha mchezo wa mataifa mengine,'' alisema kocha wake, Meshack Senge. Aliongeza kuwa kwanza watashiriki mechi mbili za kirafiki dhidi ya klabu za nchini humo kupima uwezo wa wachezaji wake. Alidokeza kuwa wamejipanga kuonyesha uwezo wao huku wakiwa tayari kujifunza mengi kutoka kwa mataifa hufanya vizuri kama Afrika Kusini na mengine.


Orodha ya wachezaji hao inajumuisha: Ajay Dosaja, Michael Obuya, Eli Asura, Farhan Khan, Samuel Oungo, Joab Ondiro, Arif Shah, Bill Olang, Harpreet Seehra, Friday Mathews na Amritpal Ghataurhae. Wengine ni Asif Shah, Willis Okeyo, Barnabus Odhiambo, Aseem Joshi, Wycliffe Ongori, Inderjit Matharu, Parraj Sehmi, Kennedy Kyalo na Herminder Singh.

Maofisa wao: Meshack Senge (kocha), Moses Majiwa, John Fernades, Del Mudher na Ashish Sharma (daktari). Kipute hicho kitashirikisha mechi za viwango tofauti ikiwamo waliozidi umri wa miaka 35 na 40 kwa wanaume vile vile wanawake. Kategoria zingine kwa wanaume zitakuwa kwa waliozidi umri wa miaka 65, 70 na 75.



Kwa wanaume waliozidi miaka 40 shindano hilo litajumuisha timu 14 ambazo zimegawanywa katika makundi matatu. Kenya imepangwa Kundi C linaloshirikisha Ujerumani, Malaysia, Singapore na All International Masters Community (ALL IMC). Kundi A lina:Uingereza, Amerika, Afrika Kusini na Australia International Masters Community. Nalo Kundi B linajumuisha: Australia, Ufaransa, Argentina, New Zealand na Afrika Kusini International Masters Community. Safari ya timu hiyo imefadhiliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Kenya Airways, Daikyo Japan Motors, Trade Routes, Sikh Union Club, Dime Credit, Filmline Limited na Interor Inspirations Limited.

 
 
bottom of page