Luyali: Uongozi Wetu Utazingatia Uwazi, Uadilifu na Uwajibikaji
- heartmediak4
- Oct 8, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 8 Oktoba 2024

MWANIAJI wa wadhifa wa Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Kanda ya Nairobi Mashariki, Eric Luyali amewatoa rangi viongozi wanaondoka kwa kutotimiza ahadi zao katika makuzi wa mchezo huo. Amedokeza kuwa katika kipindi cha uongozi wao wamekosa kuonyesha uwazi, uadilifu na uwajibikaji. ''Nawaomba washika dau wa soka katika Kanda ya Nairobi Mashariki wakati wa uchaguzi utakaoandaliwa Mwezi Desemba mwaka huu watekeleze wajibu wao wakitilia maanani makuzi ya mchezo huo,'' anasema Luyali. Amedokeza hayo wakati wa fainali za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup zilizoandaliwa Jumapili tarehe 6, Oktoba 2024 ugani Ruben, Mukuru kwa Ruben, Embakasi Nairobi. Tangia mechi za shindano hilo zilianza hadi mwisho Luyali alichangia Sh60,000.

Mgombeaji huyo aliongeza kuwa itakuwa vizuri kwa washika dau wachague viongozi wenye maono ya kusaidia ukuaji wa soka nchini. Wakati wa fainali hizo, Luyali aliandamana na Joseph Kiragu mgombeaji wa wadhifa wa mweka hazina. Wawili hao wapo kwenye mrengo wa Hussein Mohammed ambaye ametangaza kugombea wadhifa wa mwenyekiti wa kitaifa. Mwingine ambaye amejitosa kuwania uenyekiti wa Kanda ya Nairobi Mashariki ni, Dickson Doyo aliyekuwa katibu wa kanda hiyo katika uongozi unaondoka.

Kiragu alipongeza waandalizi wa shindano la Ruben FM Cup na kutoa wito kwa waandalizi wa michuano ya mashinani wawe wakishirikisha timu nyingi za wanawake. Shindano hilo lilijumuisha timu 32 za wanaume na nane za kina dada. ''Pia itakuwa vizuri kwa waandalizi wa mashindano hayo kutuza washindi hela nzuri ili kujisaidia kwenye shughuli zao kimichezo,'' anasema. Anaongeza kuwa ili kutoa nafasi kunoa talanta za wachezaji wa viwango vya chini mashindano hayo napaswa kushirikisha timu za ligi za chini hasa kiwango cha Kaunti ndogo hadi Daraja la pili lakini sio daraja la kwanza, Supa Ligi ya Taifa (NSL) na Ligi Kuu ya FKF (FKFPL).



