Ligi ya Daraja ya Kwanza Voliboli ya Vidume Kufungua Pazia Ijumaa Hii
- heartmediak4
- Nov 14, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Alhamisi 14, Novemba 2024\

KAMPENI za ligi ya taifa daraja ya kwanza katika voliboli ya wanaume msimu huu zimeratibiwa kung'oa nanga Ijumaa hii tarehe 15 Novemba 2024 uwanjani Nyayo Stadium, Nairobi. Kwenye mechi hizo za siku tatu vidume wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) watakuwa mbioni kusaka alama tisa baada ya kuingia dimbani mara tatu.
KU ambayo hunolewa na kocha, Vitalis Ojukwu Ijumaa hii itakabili washiriki wapya Seemlaw. Kwenye mechi za Jumamosi itamenyana na Kenya Prisons Central kisha Jumapili itazipiga dhidi ya Chemasteel inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza. ''Ninaamini tumepiga tizi ya kutosha kuanza kampeni zetu kwa kushinda mechi zote,'' anasema kocha wa KU.

Hata hivyo anaongeza kuwa wanafahamu wanatarajia upinzani mkali. Kadhalika anasema itakuwa vigumu kubashiri mechi za wapinzani hasa washiriki wapya.Anadokeza kuwa katika mpango mzima wanalenga kupambana mwanzo mwisho kupigania kumaliza kati ya nafasi tano bora kama watalemewa kunasa tikiti ya kuapndishwa ngazi msimu ujao. KU inajivunia huduma za wachezaji shupavu kama Ibrahim Kiprotich, Faustine Kaiser, Frank Ondego na Stephen Otieno.
Nayo Pamoja Tujijenge ya kocha, Joseph Kimemia Ijumaa hii itashuka dimbani kuchuana na Deaf Volleyball. Mechi ya pili Pamoja Tujijenge itaivaa Micro Spikers kisha Jumapili itamalizia shughuli dhidi ya Eldoret Water. ''Kuna jambo tumegundua katika mchezo wa voliboli, kila mwaka inazidi kuimarika ambapo kamwe hatuwezi kupuuza wapinzani wetu eti kwa sababu msimu uliyopita tuliwashinda,'' anasema kocha wa Pamoja Tujijenge. Anangeza kwamba kikosi chake kimejipanga kiume kukabili wapinzani wao kama timu kubwa kwenye kampeni za muhula huu.

Mechi zingine zinazotazamiwa kushuhudia uhondo mkali itakuwa baina ya Kenya Navy na Vihiga County, Kenya Airforce (KAF) dhidi ya Eldoret Water. Vile vile Kenya Prisons Central itakayokutanishwa na Chemasteel.


