top of page
Search

Leads United Yaonyesha Mlango Kipute cha Kothbiro

  • heartmediak4
  • Nov 5, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne 5, November 2024




TIMU ya Leads United imelambishwa sakafu na Mbuta FC na kuaga mashindano ya makala ya 47 kuwania taji la Kothbiro. Leads United imepokezwa kichapo xha mabao 2-1 na Mbuta FC kwenye mechi ya raundi ya 16 bora iliyochezwa Jumatatu tarehe 4 Novemba 2023 ugani Umeme, Ziwani Nairobi. Wachana nyavu wa Mbuta FC chini ya kocha, Caleb Osodo waliteremka dimbani kwa shughuli moja, kuzaba wapinzani wao na kunasa tiketi ya kushiriki robo fainali za muhula huu.



Pia ilishusha mechi safi na kunasa bao la kwanza ndani ya kipindi cha kwanza kupitia juhudi zake Lee Ombere. Kila upande uliendelea kuonyesha ubabe wake na hatimaye kipindi cha kwanza kukamilika Mbuta ikiwa kifua mbele kwa bao 1-0. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi si haba ambapo Leads United ilionyesha kufufua mchezo wake na kusawazisha kunako dakika ya 67 kupitia juhudi zake Mark Wekesa. Bao hilo lilichochea wachezaji wa Mbuta FC na kuanza mashambulizi yao kama nyuki ambapo Mark Otieno alitinga bao la pili na kuweka Mbuta FC kifua mbele.



''Tunashukuru Mola kwa ufanisi huo ikiwa ndio mwanzo kushiriki ngarambe ya Kothbiro,'' anasema kocha wa Mbuta. Anaongeza kuwa wamepania kushiriki kila mechi kwa jinsi itakavyokuwa. Katika mpango mzima anapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha soka safi kinyume na matarajio ya wengi na kuashiria wanalengo la kubeba taji hilo maana hakuna lisilowezekana.




Kwenye mchujo Kundi A, Leads United ilimaliza ya kwanza kwa alama sita, moja mbele ya Kahliweed. Kwenye mechi za Kundi B, Mbuta iliibuka ya pili kwa alama tano huku Watch and Learn FC ikimaliza kidedea kwa alama saba. Kwenye kipute cha makala yaliyopita, Leads United ilibanduliwa katika hatua ya robo fainali.



Katika ratiba ya mechi hizo, Kamkunji FC imepangwa kukabili Black Mamba leo Jumanne tarehe 5, Novemba 2024. Kamkunji FC ilijikatia tiketi ya mechi hizo baada ya kumaliza kifua mbele Kundi C kwa kushinda mechi zote tatu na kusajili pointi tisa, tatu mbele ya Ruaraka All Stars. Black Mamba iliyokuwa imepangwa kundi D iliibuka ya pili kwa kuzoa alama tano nayo Kayole Select ilimaliza kileleni kwa alama saba.

Katika ratiba ya Jumatano tarehe 6, Novemba 2024 Omena FC itakutanishwa na Kiambiu Warriors.

 
 
bottom of page