Leads United Yanusia 16 Bora Ngarambe ya Koth Biro
- heartmediak4
- Sep 6, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa, 6 Septemba 2024
TIMU ya Leads United inakaa pazuri kutwaa tiketi ya kushiriki mechi za hatua ya 16 bora kwenye kampeni za makala ya 47 kuwania taji la koth Biro.
Leads United imepiga hatua hiyo baada ya kubamiza Kingpower FC kwa mabao 2-1 ugani Umeme Ziwani, Nairobi kwenye mechi iliyochezwa Jumatano tarehe 4, Septemba 2024.

Nayo Mlango United itahitaji kushinda mechi ya mwisho baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 na Kahliweed FC. Bao la Mlango lilifumwa kimiani na Erick Okondi huku Musa Mwangi akisawazishia Kahliweed. ''Tulipoteza alama mbili muhimu ambapo itabidi tujikaze zaidi kwenye mechi ya tatu ili tufuzu kushiriki mechi za 16 bora,'' anasema kocha wa Mlango United, James Mwangi. Anaongeza kuwa wamejifunza mengi kutokana na mechi hizo mbili.
Leads United ambayo imepangwa Kundi A ilipata mabao hayo kupitia juhudi zake Issa Ochora na Richard Omondi. Nalo bao la kufutia machozi la Kingpower FC lilifungwa na Levis Mbonyo. Kwenye patashika iliyochezwa Alhamisi tarehe 5, Septemba 2024, Mbuta FC ilibeba ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Shauri Moyo. Calistus Miheso na Victor Kasero wa Mbuta FC kila mmoja alitikisa wavu mara moja na kusaidia kuzoa alama tatu muhimu. Nalo goli la Shauri Moyo lilifumwa kimiani na Kamei Nakusanya.

Kwenye mfululizo wa kipute hicho mechi mbili zimepangwa kuchezwa Jumamosi hii tarehe 7, Septemba 2014. Katika ratiba ya Kundi D, Napoli Comrade itapepetana na Macmillan Seniors huku Kamkunji FC ikikutanishwa na Ruaraka All Stars kwenye mechi za Kundi C.
Pumwani Sportiff iliyoanza kampeni zake kwa kutoka sare tasa dhidi ya Kiambiu Warriors ndio mabingwa watetezi. Kwenye mechi za makala ya 44 Leads United ilimaliza ya pili iliponyukwa mabao 4-2 na Korongez kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali. Kwenye makala ya 45 mshindi alikosekana pale wafuasi wa Borussia FC walipozua fujo baada ya kikosi hicho kutoka sare tasa na Leads United.


