Leads United Yaadhibu Mlango United Ngarambe ya Koth Biro
- heartmediak4
- Aug 27, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 27 Agosti 2024.
LEADS United imefungua kampeni zake vyema kwenye mbio za kuwania makala ya 47 taji la Koth Biro baada ya kuadhibu Mango United kwa bao 1-0 mnamo Jumatatu tarehe 26 Agosti ugani Umeme Ziwani, Nairobi. Vikosi hivyo vilionyesha ushindani mkali ambapo ndani ya kipindi cha kwanza vilitoka sare tasa.
Kipindi cha pili kilianza kwa kishindo huku Leads United ya kocha Issa Winston ikivuruga lango la wapinzani wao ikiwinda kupata ushindi. Juhudi za wachezaji hao zilipata matunda pale Issa Ochera alipotikisa wavu kwa kutupia kimiani kombora zito. Bao hilo lilichochea wapinznai wao ambapo wazinduka na kuanza kuvamia lango la Leads kama nyuki.

Lango la Leads lilikuwa kama uwanja wa vita ambapo Mlango ya kocha, James Mwangi ilikuwa ikiwinda bao kwa udi na uvumba. Mlinda lango wa Leads aliibuka mkombozi pale alipozuia mikwanju mikali mara tatu.
Kwenye mshikemshike huo Shueb Mahd wa Mlango United alichezea mwenzake vibaya na kulambishwa kadi nyekundu. ''Kiasi hatukuwa tumejipanga vizuri maana tulishuka dimbani muda mchache tulipokusanyika pamoja kwa mara ya kwanza baada ya kuchukua breki ya muda,'' anasema kocha wa Leads.
Anaongeza kwamba ratiba ya kipute hicho iliachiliwa kuchelewa hali iliyowakuta bila kutarajia. Anadokeza kuwa sasa wameanza kupiga hesabu ya michuano hiyo ambapo lazima wapige tizi kali kujinolea michuano ijayo. Kadhalika anakiri kuwa endapo wamepania kufanya kweli kwenye kampeni za msimu huu lazima warekebishe makosa yao. Leads ya sasa inajumuisha vijana wadogo na wapya.

Kwenye makala yaliyopita Leads ilibanduliwa katika hatua za robo fainali.
Naye kocha wa Mlango United anapongeza vijana wake kwa kujituma kwa udi na uvumba licha ya bahati kutosimama. ''Vijana wangu walionyesha soka nzuri hasa katika kipindi cha pili ila hawakubahatika kupata bao,'' anasema. Anaongeza kwamba itabidi warekebishe makosa yao kwenye mechi zijazo.
Katika ratiba ya kipute hicho kesho Jumatano tarehe 28 Agosti, Black Mamba itapepetana na Dandora Derby nayo Biafra Kamaliza itakutanishwa na Ruaraka All Stars. Pumwani Sportiff ndio mabingwa watetezi. Kwenye mechi za makala ya 44 Leads United ilimaliza ya pili iliponyukwa mabao 4-2 na Korongez kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali.
Kwenye makala ya 45 mshindi alikosekana kufuatia hatua ya wafuasi wa Borussia FC kuzua fujo baada ya kikosi hicho kutoka sare tasa na Leads United.



