top of page
Search

Koth Biro: Ziwani All Stars Itahitaji Kuzima Pumwani Sports Ili Kufuzu

  • heartmediak4
  • Sep 10, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 10 Septemba 2024


ZIWANI All Stars imekaa vizuri kufuzu kwa mechi za raundi ya 16 bora kwenye kampeni za makala ya 47 kuwania taji la koth Biro. Hata hivyo itahitaji kuangusha Pumwani Sports Club kwenye mechi ya mwisho ya mchujo Kundi F.

Kocha wake, John Otieno amesema hayo baada ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya Kiambiu Warriors kwenye mechi iliyochezwa Jumatatu tarehe 9, Septemba 2024 ugani Umeme Ziwani, Nairobi.



Kiambiu Warriors ilitangulia kufunga kupitia Lewis Shivachi kabla Magadi Ali kusawazishia Ziwani All Stars. Kisha Shivachi alifungia Kiambiu bao la pili. Kunako dakika za mwisho Ziwani All Stars ilisawazisha kupitia juhudi zake Lameck Luhangala. ''Tumekaa pazuri kufuzu kwa raundi ya 16 bora lakini tumepania kupambana mwanzo mwisho kwenye mechi ya mwisho ili kutwaa tiketi ya kufuzu moja kwa moja,'' anasema kocha wa Ziwani All Stars. Anaongeza kuwa pambano lao na Pumwani Sports Club litakuwa kama fainali kabla ya fainali kamili.


Kwenye utangulizi wa mechi hizo, Ziwani Allstars ilipiga Eastleigh Stars mabao 2-0, nayo Pumwani Sports Club ilitoka sare tasa dhidi ya Kiambiu Warriors kabla ya kupiga Eastleigh Stars kwa mabao 2-0. Mabao hayo yalipatikana kupitia Mosaa Mohammed na Mohammed Khalili.. Katika jedwali la kundi hilo Ziwani All Stars imetua kileleni kwa alama nne sawa na Pumwani Sports tofauti ikiwa idadi ya mabao.


Kwenye matokeo hayo, Watch and Learn FC ilisajili ushindi wa pili ilipodunga Ajax Rock City bao 1-0 kupitia juhudi zake Evans Juma. ''Tuna imani tunatosha mboga kufanya kweli wala hatuna hofu dhidi ya wapinzani wetu bali tunalenga kunasa tiketi ya mechi za raundi ya 16 bora,'' anasema kocha wa Watch and Learn, Abdi Naja. Anaongeza kuwa kwenye mechi ya mwisho watahitaji ushindi ama kutoka nguvu sawa ili kutimiza amza yao.




Nao Kelly Ndululu na Gilly Nyange kila mmoja aliachia kombora moja na kubeba Omena FC kuzaba Macmillan Junior mabao 2-1. Goli la kufutia machozi la Macmillan lilifunikwa kimiani na Charles Njuguna. Kocha wa Macmillan, Brian Odhiambo anasema kuwa lazima washinde mechi ya mwisho dhidi ya Kamkunji Falcons ili kunasa tiketi ya kusonga mbele.

 
 
bottom of page