Koth Biro: Timu 3 Kusubiri Mwaka 1 Kuwania taji hilo
- heartmediak4
- Sep 18, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Alhamisi, 18 Septemba 2024
TIMU ya Mlango, Shauri Moyo Sporiff na Kingpower FC zimetanguliwa kubanduliwa kwenye mechi za makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro.
Mlango ya kocha, James Mwangi imeondokea kipute cha mwaka huu baada ya kutoka nguvu bao 1-1 na Kingpower kwenye patashika ya mwisho Kundi A iliyochezwa Jumamosi. Kingpower ilitangulia kufungiwa na Lexian Ochieng kisha Erick Okodoi alisawazishia Mlango.

Mlango imeibuka ya nne Kundi hilo kwa kuzoa alama mbili baada ya kutoka nguvu sawa mara mbili kwa bao 1-1 kila moja dhidi ya Kahliweed na Kingpower. Kwenye mechi ya tatu ilidungwa goli 1-0 na Leads United. ''Tumekubali yaishe licha ya kamba hatujatiiza azma yetu kuendelea na shindano la mwaka huu,'' kocha wa Mlango alisema. Aliongeza kwamba sasa watasubiri kujaribu tena kwenye mechi za makala ya mwaka ujao.
Kwenye mechi ya Kundi B, Shauri Moyo ilinyukwa mabao 3-1 na Ajax Rock City. Wafungaji wa Ajax Rock City walikuwa Llyod Onyango aliyetikisa wavu mara mbili naye Stephen Ochieng aliyefunga bao moja.

Matokeo hayo yamefanya Shauri Moyo Sportiff kubanduliwa baada ya kumaliza nafasi ya nne Kundini. ''Tunashikilia nafasi ya pili Kundini ambapo tunashikilia mikono tukiomba angalau Watch na Learn FC ishinde Mbuta FC ili tufuzu kushiriki mechi za robo fainali,'' alisema kocha wa Ajax, Joseph Morte. Aliongeza kuwa Mbuta FC ikishinda Watch and Learn hatutakuwa na budi ila tutabanduliwa kwenye mechi za mwaka huu.
Kwenye mechi za makala yaliyotangulia Leads United ilimaliza ya pili ilipozabwa mabao 4-2 na Korongez FC kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali. Kwenye ngarambe ya mwaka 2021 mshindi alikosekana kufuatia hatua ya wafuasi wa Borussia FC kuzua fujo baada ya kikosi hicho kutoka sare tasa na Leads United. Shindano hilo ni kati ya michuano ambayo hushirikisha wachezaji wa klabu za ligi tofauti hapa nchini.


