Koth Biro: Ruaraka All Stars Yararua Biafra Kamaliza
- heartmediak4
- Aug 29, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Alhamisi, 29 Agosti 2024
TIMU ya Ruaraka All Stars imekomoa Biafra Kamaliza FC kwa mabao 3-0 kwenye mechi za makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro iliyochezwa Jumatano tarehe 28 Agosti ugani Umeme Ziwani, Nairobi. Biafra Kamaliza FC kocha, Cyril Peter ilipata ushindi huo kupitia juhudi zake Tyson Odhiambo, Erick Kipkurui na Raphael Omondi waliotikisa wavu mara moja kila mmoja.

''Ninapongeza wachezaji wangu kwa kazi nzuri waliofanya kupata mwanzo mzuri ambapo tayari umetupatia motisha ili kutia bidii kwenye mechi zijazo,'' kocha wa Biafra Kamaliza anasema. Anongeza kuwa wachezaji wake walizoa ufanisi huo baada ya kufuata mawaidha ya viongozi wao vyema. Anasisitiza kuwa ni muhimu kuanza vyema kampeni zetu ili kupata tumaini la kusonga mbele kwanza kufuzu kwa mechi za hatua ya 16 bora.
Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Kamkunji FC ilinyamazisha Gikomba All Stars kwa kuipiga bao 1-0. Bao hilo lilitupiwa kimiani na Reagan Meme.
Nayo Mbuta FC ilitoka sare tasa dhidi ya Ajax Rock City.

Kwenye ratiba ya michuano hiyo Ijumaa tarehe 30 Agosti,Taawun FC ya kocha, Stephen Ochieng itashuka dimbani kukabili Kariadudu FC. Nao wanasoka wa Macmilan Senior FC watachuana na Kayole Select. ''Ninachofahamu ni kuwa lazima tujitume kiume ili tuanze mechi zetu kwa kishindo hasa kuzoa pointi tatu muhimu kusudi tujiweke pazuri kwenye juhudi za kufukuzia tiketi ya kusonga mbele,'' anasema kocha wa Taawun. Anaongeza kuwa wanafahamu wapinzani wao wamejipanga kuwalipua ili kujiweka pazuri kusonga mbele. Pumwani Sports ndio mabingwa watetezi. Pumwani Sports ni kati ya timu 22 ambazo hushiriki michuano ya FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL). Kwenye mechi za makala ya 44 Leads United ilimaliza ya pili iliponyukwa mabao 4-2 na Korongez kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali.
Kwenye makala ya 45 mshindi alikosekana kufuatia hatua ya wafuasi wa Borussia FC kuzua fujo baada ya kikosi hicho kutoka sare tasa na Leads United.


