top of page
Search

Koth Biro: Robo Fainali Wacha Katambe

  • heartmediak4
  • Nov 13, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumatano, 13 Novemba 2024.


KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa kwenye mechi za robo fainali za makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro zitakaopigiwa ugani Umeme Ziwani, Nairobi. Mechi za robo fainali zimeratibiwa kuchezwa Alhamisi hii na Ijumaa hii (tarehe 14 Novemba na 15 Novemba mtawalia).


Kwenye ratiba ya Alhamisi hii, Watch and Learn FC ya kocha, Bonface Omino imepangwa kucheza na Kayole Select FC nao wanasoka wa Mbuta FC watakabili Kamkunji FC. Kwenye ratiba ya Ijumaa, Kiambiu Warriors itaumana na Kariadudu mwisho mabingwa watetezi, Pumwani Sports watakutanishwa na Mathare Combined.


Watch and Learn inapigiwa chapuo kupambana kiume kusaka tikiti ya nusu fainali. ''Bila shaka tumepania kujituma kwa udi na uvumba kuhakikisha tunasonga mbele,'' anasema kocha wa Watch and Learn FC. Anaongeza kuwa ndio mwanzo kushiriki kipute hicho lakini wanataka kubeba taji la msimu huu. Kufikia sasa Watch and Learn FC haijapoteza mechi yoyote. Kwenye mechi za makundi ilishinda mechi mbili na kutoka nguvu sawa mara moja.




Kocha wa Mbuta, Caleb Osodo anasema ameandaa vijana wake tayari kuonyesha soka safi huku wakilenga kufanya kweli ili kusonga mbele. ''Ninaamini wachezaji wangu wanatosha mboga kulipua wapinzani wetu na kujikatia tikiti ya nusu fainali,'' alisema kocha wa Mbuta FC. Aliongeza kuwa wengi hawakutarajia kikosi chake kizamishe Leads FC lakini dakika tisini ziliamua. Anashikilia kuwa ingawa hawawezi kupuuza wapinzani wao pia nao wasiwadharau.


Kwenye mechi za raundi ya 16 bora, Watch and Learn FC ilizaba Kahliweed FC kwa mabao 3-0 nayo Kayole Select ilizoa ushindi wa mezani dhidi ya Ruaraka All Stars. Nayo Mbuta FC ilinyuka Leads United mabao 2-1 huku Black Mamba ikizabwa bao 1-0 na Kamkunji FC.


Kiambiu Warriors iliadhibu Omena FC kwa mabao 2-0, Kariadudu iliangusha Mbotela Kamaliza kwa magoli 4-1. Mathare Combined ilicharaza Tawuun FC kwa mabao 3-1 nayo Pumwani Sports ilipata ushindi mwepesi wa mabao 3-2 mbele ya Kakuma Stars.

Mshindi wa kipute cha mwaka huu atatuzwa Sh100,000, nafasi ya pili atapata Sh50,000 huku timu zitakaomaliza nafasi ya tatu na nne zikipongezwa kwa Sh30,000 na Sh10,000 mtawalia

 
 
bottom of page