Koth Biro: Kiambiu, Ziwani Allstars Kundi Moja na Mabingwa Watetezi Pumwani Sports.
- heartmediak4
- Aug 21, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Jumatano, 21 Agosti 2024
MABINGWA watetezi kwenye taji la Koth Biro, Pumwani Sportiff wamepangwa Kundi F kwenye kampeni za ngarambe ya makala huu ambayo imepangwa kung'oa nanga Jumamosi hii tarehe 24 Agosti.

Kulingana na droo ambayo imefanywa Jumatano tarehe 21 Agosti kwenye uwanja wa Umeme Ziwani, Nairobi mabingwa watetezi hao wamepangwa kundi moja na Kiambiu Warriors, Ziwani Allstars na Eastleigh Stars. ''Bila shaka kundi hilo litashuhudia ushindani mkali kwenye kampeni za muhula huu,'' anasema ofisa mkuu wa kamati andalizi ya kipute hicho, Issa Barugote. Hata hivyo anaongeza kuwa kwa jumla hakuna timu ya kupuuza maana michuano hiyo inatazamiwa kushuhudia upinzani wa kufa mtu. Kwenye makala yaliyopita, Ziwani Allstars, Kiambiu Warriors na Eastleigh Stars zilibanduliwa katika hatua za robo fainali.
Wakali wengine, Leads United wamepangwa Kundi A linalojumuisha Mlango FC, African Warriors na Ngara Sportiff. ''Kulingana na droo ya mechi za mwaka huu ni kweli hatuwezi kupuuza wapinzani wetu lakini kitaeleweka maana lazima tupambane kwa udi na uvumba kupigania tiketi ya kusonga mbele,'' anasema kocha wa Leads, Winston Issa. Kwenye mechi za makala yaliyotangulia Leads United ilimaliza ya pili iliponyukwa mabao 4-2 na Korongez kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali.

Kwenye ngarambe ya mwaka 2021 mshindi alikosekana kufuatia hatua ya wafuasi wa Borussia FC kuzua fujo baada ya kikosi hicho kutoka sare tasa na Leads United. Shindano hilo ni kati ya michuano ambayo hushirikisha wachezaji wa klabu za ligi tofauti hapa nchini.


