top of page
Search

Koth Biro: Kiambiu Warriors, Mathare Commbann Zatinga Fainali Mwaka Huu

  • heartmediak4
  • Nov 25, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumatatu 25, Novemba 2024.


MATUMAINI ya Mbuta FC kunasa tikiti ya fainali ya makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro yamegonga ukuta baada ya kuzimwa na Kiambiu Warriors kwenye nusu fainali iliyochezwa Jumatatu tarehe 25, Novemba 2024 uwanjani Umeme Ziwani, Nairobi.

Timu zote zilishuka dimbani kwa makeke zikiwinda ushindi ili kufuzu kwa fainali ya mwaka huu. Mbuta FC ya kocha, Caleb Osodo ilitangulia kufunga dakika ya 20 kupitia Mark Wekesa kabla ya Eugene Otieno kusawazishia Kiambiu Warriors dakika tano baadaye. Kipindi cha kwanza kilikamilika matokeo yakiwa bao 1-1. Kipindi cha pili vikosi vyote vilirejea uwanjani tayari kufanya kweli. Mvua ilikuwa iinaendelea kunyesha hali iliyochangia kuwa vigumu mechi kuchezeka kwa sababu ya maji. Hata hivyo Kiambiu ilionyesha mchezo wa hali yajuu kuliko wapinzani wao.


Huku ikiwa imesallia dakika kumi mchezo kutamatika, Victor Otieno alifungia Kiambiu Warriors bao la ushindi. ''Kwa neema zake Mungu tumetinga fainali ya mwaka huu,'' anasema kocha wa Kiambiu. Anaongeza kuwa wachezaji wake walijituma kwa udi na uvumba ndio wakapata matokeo mazuri. Anadokeza kuwa haikuwa rahisi kwa kuzingatia ndio mwanzo kuongeza kikosi hicho na wamefanikiwa kutwaa tikiti ya fainali. Anashikilia kuwa wapo tayari kushiriki fainali ambapo wanatarajia kubeba taji la mwaka huu.



Naye kocha wa Mbuta FC alikubali yaishe na kusema kuwa walifanya vizuri maana ndio wamepoteza mechi ya kwanza kwenye kampeni za mwaka huu.

''Mechi ya nusu fainali ilikuwa Koth Biro halisi maana uwanja ulikuwa umeloa maji,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kwamba vijana wake walijituma kiume lakini bahati haikusimama na kwa mechi yoyote lazima iwe na mshindi.






Mwenyekiti wa shindano hilo, Issa Musa anasema mechi za mwaka huu zilikuwa nzuri bila visa vingi vya utovu wa nidhamu ambapo sasa wanaelekea tamati.

''Katika mpango mzima tuna tatizo ambapo bado tunasaka mdhamini angalau tuweze kutuza washindi wa kipute cha mwaka huu,'' anasema. Anangeza kuwa milango iwazi kwa yoyote anayeweza kuwapiga jeki.



Nayo Mathare Commban ilitwaa tikiti ya fainali baada ya kuchapa Watch na Learn FC kwa mabao 7-6 kupitia mipigo ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1.

''Ninapongeza wachezaji wangu kwa kujituma na kubeba tikiti ya fainali lakini haikuwa mteremko,'' anasema kocha wa Mathare Commbanb. Anaongeza kwamba ana imani mwaka huu watawazwa mabingwa wapya. Pia alipongeza Watch and Learn FC kwa kuwapatia upinzani mkali.


Kwenye robo fainali atch and Learn FC ilikung'uta Kayole Select FC kwa mabao 3-1. Nayo Mbuta FC ilinyuka Kamkunji FC kwa bao 1-0, Mathare Commban ilishinda Pumwani Sports Club iliyokuwa bingwa mtetezi kwa mabao 2-1 huku Kiambiu Warriors FC ikibeba ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Kariadudu FC.

Watch and Learn FC inajivunia kutwaa taji la The Rissa Football Tournament. Katika fainali Watch and Learn iliangusha Tabiban FC kwa mabao 4-2 katika fainali baada ya kurarua Villaroma FC kwa mabao 5-1 kwenye nusu fainali.


 
 
bottom of page