top of page
Search

Kivumbi Kikali Kushushwa Wikendi Michuano ya Ruben FM Cup

  • heartmediak4
  • Aug 16, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 16 Agosti 2024


KIVUMBI kikali kinanukia wikendi hii (Jumamosi na Jumapili) kwenye kampeni za kufukuzia ubingwa wa makala ya saba ya taji la Ruben FM Cup huku zikitinga wiki ya pili.


Jumamosi hii tarehe 17 Agosti 2024, Young Warriors imepangwa kuialika Free Pentecostal Fellowship in Kenya (FPFK) ugani Vision Mukuru kwa Njenga, Embakasi. Nayo Barca Veteran itakuwa ugani Embakasi Girls kukabili NAS FC. Barca itakuwa ikiwinda ushindi wa kwanza baada ya kupigwa mabao 2-1 na Corinthians FC wiki iliyopita.




NAS itashuka dimbani huku ikijivunia kuangusha Embakasi East FC kwa bao 1-0 wiki iliyopita. Ruben United itaingia mzigoni ugani Ruben kucheza na Meteorite FC huku kila moja ikiwinda ushindi wa kufungua vyema kampeni zake.


Jumapili tarehe 18 Agosti 2024, Nyati FC ya kocha, Michael Wanjohi itateremka dimbani uwanjani Vision kutifua vumbi dhidi ya Amusha FC. ''Hatuna lingine tumepania kuzima ndoto ya wapinzani wetu na kuzoa alama tatu muhimu kwenye juhudi za kufukuzia azma yetu ya kufuzu kwa raundi ya pili,'' anasema kocha wa Nyati FC. Anaongeza kuwa wanafahamu bayana wapinzani wao pia wameandaa mamluki wao tayari kuwanyamazisha.




Hata hivyo anashikilia dakika tisini ndizo zitakaoamua nani bingwa kwenye mchezo huo. Nyati FC itakuwa kazini kusaka ushindi wa pili baada ya kusajili mabao 2-0 mbele ya Deportivo Leon FC wiki iliyopita. Nyati inategemea huduma za wapiga gozi matata akiwamo Elvis Omolet, Elvis Mboya, Kelvin Okech, Felix Ochieng, Jesse Inanga na Rodgers Tangasi.


Naye kocha, Silas Kivasu ataiongoza Corinthians FC kumenyana na Embakasi East kupigania ushindi wa pili. ''Tumepania kushusha soka la kibiashara ili kujiongezea tumaini la kusonga mbele,'' anasema kocha wa Corinthians. Anaongeza kuwa wanafahamu wazi kuwa mchezo huo hautakuwa mteremko. Corinthians itategemea kasi ya wachezaji wake akiwamo Alex Mutinda (nahodha), Brian Iwobi, Denis 'Lefty', Aron Kimanzi, John Andere na Analo Steven kati ya wengine.


Nayo Kamongo FC ya kocha Enock Mukoma itashuka ugani Vision kuchuana na Creative Hands. ''Tunaelewa kuwa wapinzani wetu sio wachache kwa kuzingatia walimaliza nafasi ya pili kwenye mechi za makala yaliyopita ambapo lazima tuwe makini zaidi,'' anasema. Hata hivyo anadokeza kwamba kamwe hawawezi kuuziwa uoga wanaume ni kuonana. Kamongo inajivunia wanasoka hodari kama Anthony Kyale, Edwin Maina, Daniel Simiyu, Joseph Wamalwa, Kelvin Mutua na James Juma.


Kwenye ratiba hiyo, Simba FC itakwaruzana na BUSEC FC, Milan itaumana na Gateway FC, Minto FC itaivaa Deportivo FC, Mukuru Wazee itachuana na mabingwa watetezi, Shofco FC huku Tala Allstars ikikutanishwa na Vision FC.

 
 
bottom of page