Kivumbi Kikali Kinanukia Robo Fainali Ruben FM Cup
- heartmediak4
- Sep 21, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumamosi,21 Septemba 2024
KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa Jumapili hii tarehe 22 Septemba 2024 kwenye mechi za kitengo cha wanaume za robo fainali za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup ugani Ruben, Mukuru Kwa Ruben, Embakasi Nairobi.
Kocha, Catherine Muoka ataongoza Meteorite FC huku wakilenga kuendeleza ubabe wao watakapokabili Mukuru Wazee FC. ''Bila shaka tunalenga kuendelea kufana kwenye kampeni za mwaka huu kwani tayari tumeshinda mechi zote nne ambazo tumshiriki,'' kocha huyo anasema. Anaongeza kuwa licha ya kujiwekea tumaini hilo wanafahamu mechi hiyo haitakuwa mteremko maana wapinzani wao pia hawakufuzu kwa kiwango hicho kibahati bali walijituma kwa udi na uvumba. Meteorite inajivunia huduma za wachezaji shupavu kama Philip Omasaja na Sylvester Patrick kati ya wengine.

Meteorite iliyoshinda mechi tatu za mchujo ilifuzu kwa robo fainali baada ya kuzoa ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Corinthians kwenye mechi za raundi ya 16-Bora. Nayo Mukuru Wazee FC ilizamisha Amusha FC kwa mabao 8-7 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka sare tasa.
Wilson Aviators FC inayoshiriki ngarambe hiyo kwa mara ya kwanza itamenyana na Kamongo FC. ''Tunaelewa mechi hiyo haitakuwa mteremko lakini tumejipanga kiume kuonyesha ubabe wetu kwani tumepania kutetemesha wapinzani wetu na kusonga mbele,'' anasema nahodha wa Wilson Aviators, Sylvester Lichama. Anaongeza kwamba wamepania kufanya kweli ili kuwaibisha wengi ambao wamekuwa wakizingua mitandaoni. Wilson Aviators inashirikisha wachezaji wepesi kama Reyvans Kinesi, Hanington Kahi, Allan Chekaya, Brian Mwania bila kuweka katika kaburi la sahau Sylvester Lichama.

Kwenye mechi za raundi ya 16-bora, Wilson Aviators ilizaba Green Santos kwa magoli 2-1 nayo Kamongo FC ililemea Real Warriors kwa mabao 4-2 kupitia mipigo ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1.
Kwenye ratiba hiyo, Vision FC itachuana na Ruben United nayo Young Warriors itakabili Creative Hands. Vision FC ilipata tiketi hiyo ilipozaba Nyati FC kwa bao 1-0, Ruben United ilipiga Nas S kwa kwa magoli 3-2 huku Creative Hands ikisajili magoli 3-0 mbele ya United Kings.
Mshindi wa kitengo cha wanaume mwaka huu atatuzwa Sh100,000. Timu itakayoibuka nafasi ya pili itapokea Sh70,000 kisha nafasi ya tatu na nne zitapongezwa kwa Sh40,000 na Sh20,000 mtawalia.


