Kipute cha Ruben FM Cup Kupata Bingwa Mpya Msimu huu
- heartmediak4
- Oct 1, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 1 Oktoba 2024

SHINDANO la kuwania taji la Ruben Cup la makala ya saba kitengo cha wanawake msimu huu linatarajiwa kupata bingwa mpya timu ambayo haikuwahi shiriki michuano hiyo. Hili ni baada ya timu zilizowahi kushiriki tena pia zilizopigiwa chapuo kutesa muhula huu kubanduliwa na vikosi limbukeni.
Mabingwa watetezi, Embakasi South Ladies United na Macmillan zilibanduliwa kwenye mechi ya mwisho ya mchujo na nusu fainali mtawalia. Kwenye nusu fainali Kipchirchir Limo aliongoza St Josephs Starlets kunyamazisha Macmillan Queens kwa kuidunga mabao 2-1. Embakasi South Ladies United iliyokuwa inajivunia kubeba taji hilo mara mbili ilitolewa ilipozabwa bao 1-0 na Kamongo Starlets kwenye mechi ya mwisho ya mchujo.
Kwenye nusu fainali ya pili, Desert Venom FC ililemea Kamongo Starlets kwa mabao 5-4 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida.

St Josephs Starlets ilipata ushindi huo kupitia juhudi zake Juliet Kemunto na Fatuma Mohammed. ''Sina shaka kupongeza wachezaji wangu mwalifanya kazi nzuri kuhakikisha tumefuzu kushiriki fainali za kipute cha mwaka huu,'' anasema kocha wa St Josephs Starlets. Anaongeza kuwa timu hufanya vizuri kupitia ushirikiano na kuelewana vyema dimbani. Anataja baadhi ya wachezaji waliosaidia pakubwa kikosi hicho kufanya kweli akiwamo Sheril Atieno (nahodha), Ivy Norah, Judy Akumu, Fatuma Mohammed na Patience Waithera. Kwa wanawake shindano la mwaka huu lilivutia timu nane.Bingwa wa mwaka huu atatuzwa Sh40,000, nafasi ya pili atapokea Sh25,000, nafasi ya tatu na nne zitatuzwa Sh15,000 na Sh10,000 mtawalia.


