top of page
Search

Kiambiu Warriors Yakanyanga Omena FC Kipute cha Koth Biro

  • heartmediak4
  • Nov 8, 2024
  • 1 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 8 Novemba 2024



TIMU ya Kiambiu Warriors imejiunga na Kamkunji Falcons pia Mbuta FC katika orodha ya vikosi ambavyo vimejikatia tikiti ya kushiriki robo fainali za makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro.

Kiambiu Warriors imesonga mbele baada ya kurarua Omena FC kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya hatua ya 16 bora iliyochezewa uwanjani Umeme Ziwani, Nairobi, Jumatano jioni(tarehe 6 Novemba 2024). Kiambiu Warriors ilishusha soka safi na kuashiria imepania kupambana kiume kwenye jitihada za kuwania taji hilo. Wachana nyavu wa kikosi hicho walipata ufanisi huo kupitia juhudi zake Otieno Boris aliyetikisa wabu mara mbili.


Kiambiu ilifuzu kwa hatua ya 16 bora baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye mechi za Kundi F kwa kusajili alama tano. Nayo Omena FC iliibuka kileleni Kundi E kwa alama tisa, tatu mbele ya Kakuma Stars. Kwenye mechi nyingine ya kiwango hicho, Ali Maleche alitikisa wavu mara moja na kubeba kamkunji Falcons kuzaba Black Mamba kwa bao 1-0.

Kamkunji ilijikatia tiketi ya mechi hizo baada ya kumaliza kifua mbele Kundi C kwa kushinda mechi zote tatu na kusajili pointi tisa, tatu mbele ya Ruaraka All Stars.

Black Mamba iliyokuwa imepangwa kundi D iliibuka ya pili kwa kuzoa alama tano, nayo Kayole Select ilimaliza kileleni kwa alama saba. Pumwani Sports ndio mabingwa watetezi baada ya kubeba taji la makala ya 46.

 
 
bottom of page