Kenya, Sinapore Kitaeleweka Kombe la Dunia la Hoki ya Masters Jumatano hii.
- heartmediak4
- Oct 15, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne 15, Oktoba 2024

TIMU ya taifa ya wanaume kwa waliozidi umri wa miaka 40 Jumatano hii tarehe 16, Oktoba 2024 itaingia mzigoni kucheza mechi ya tatu dhidi ya Singapore kwenye kampeni za Kombe la Dunia la hoki ya Masters zinazoendelea jijini Cape Town, Afrika Kusini.
Kikosi hicho cha kocha, Meshack Senge kitashuka dimbani kuwinda ushindi wa kwanza baada ya kuzabwa mabao 2-1 na Malaysia na kutoka sare tasa dhidi ya Alliance International Masters Community (Alliance IMC). ''Lazima tushinde mechi hiyo ili tujiongezea tumaini la kufuzu kwa robo fainali,'' kocha huyo anasema.
Anaongeza kuwa baadhi ya timu zinazoshiriki ngarambe hiyo zina uzoefu wa mechi za kimataifa ilhali Kenya ndio inashiriki mara ya kwanza. Anadokeza kuwa wamepata mtihani mgumu lakini anaamini wanaendelea vyema hasa baada ya kutofungana na Alliance IMC. Kando na kitengo cha waliozidi miaka 40 kwa wanaume na wanawake shindano hilo limevutia timu za wanaume waliozidi umri wa miaka 65, 70 na 75. Timu ya Kenya inajumuisha wachezaji kama:

:Ajay Dosaja, Michael Obuya, Eli Asura, Farhan Khan, Samuel Oungo, Joab Ondiro, Arif Shah (nahodha), Bill Olang, Harpreet Seehra, Friday Mathews na Amritpal Ghataurhae. Wengine ni Asif Shah, Willis Okeyo, Barnabus Odhiambo, Aseem Joshi, Wycliffe Ongori, Inderjit Matharu, Parraj Sehmi, Kennedy Kyalo na Herminder Singh.
Kitengo cha wanaume waliozidi miaka 40 kinashiriki timu 14 ambazo zimepangwa kwa makundi matatu. Kenya ipio Kundi C linaloshirikisha Ujerumani, Malaysia, Singapore na Alliance International Masters Community (ALL IMC). Kundi A lina:Uingereza, Amerika, Afrika Kusini na Australia International Masters Community. Nalo Kundi B linajumuisha: Australia, Ufaransa, Argentina, New Zealand na Afrika Kusini International Masters Community.Safari ya timu hiyo imefadhiliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Kenya Airways, Daikyo Japan Motors, Meximed International (K) Limited, ACK Autopix, Trade Routes, Sikh Union Club, Dime Credit, Filmline Limited na Interor Inspirations Limited.



