top of page
Search

Kariobangi Yazima Makeke ya RYSA na Kuibuka Wafalme wa Soka la Nairobi (NRL).

  • heartmediak4
  • Sep 3, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 3 Septemba 2024



KARIOBANGI Legends Youth imekomoa Runda Youth Sports Association (RYSA) katika fainali ya Ligi ya Kanda ya Nairobi (NRL) mwaka 2024 iliyopigwa Jumapili tarehe 1, Septemba 2024 ugani Dandora Stadium, Nairobi. Kariobangi ya kocha, Geoffrey Wangalwa na Jeremiah Akhayo ndio wafalme wa kipute hicho baada ya kufurusha RYSA kwa mabao 8-2.


Hata hivyo wachezaji wa timu zote wametwaa tiketi ya kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya Pili msimu ujao. Kariobangi ilikutanishwa na RYSA baada ya kuibuka mabingwa wa Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) na Kanda ya Nairobi Magharibi (NWRL) mtawalia. Katika fainali vijana wepesi wa Kariobangi walitandaza soka safi na kuhakikisha wanaendeleza ubabe wao.


Kariobangi ilipata ufanisi huo kupitia George Karani, Victor Kinyili na Bramwel Kavaya waliotikisa wavu mara mbili kila mmoja. Nao Robbie Maangi na Laurence Otieno kila mmoja alitupia kimiani goli moja. Upande wa RYSA ya makocha, Stanley Numi na Bonface Amudala ilipata mabao ya kufutia machozi kupitia juhudi zake Simon Gikurumi na Samuel 'Ras' Indiego kila mmoja alipotupia kimiani kombora moja.



'Sina budi kupongeza vijana wangu kwa kazi nzuri waliofanya kwenye kampeni za muhula huu na kuhakikisha wametimiza azma yetu kusonga mbele,'' anaema mwanzilishi wa Kariobangi, Eric Atanga Otieno. Anaongeza kuwa wapinzani hao walisoma nembo katika mchezo huo. Naye mwanzilishi wa RYSA, Peter Maina Mukei anasema wana furaha tele kwa kuzoa tiketi ya kupandishwa daraja licha ya kutoibuka wafalme wa ngarambe ya NRL. ''Ninachofahamu ni kuwa haikuwa mteremko lakini tunatabasamu kutokana na jacho yetu,'' anasema. Anaongeza wanafahamu wanakoenda kutakuwa moto wa kuotea mbali.





Victor Kinyili na Samuel 'Ras' Indiego waliibuka wafungaji kwa Kariobangi na RYSA mtawalia. Kariobangi iliibuka mabingwa wa NERL kwa alama 110 nayo Lucky Summer ilimaliza ya pili kwa kutia kapuni pointi 94. Nafasi ya tatu iliwaendelea wanasoka wa Babadogo United kwa pointi 87, tatu mbele ya Utawala Youth huku Automech kwa kuzoa alama 72 ikifunga tano bora.

Katika ligi ya NWRL, RYSA ilimaliza kifua mbele kwa alama 115 huku Nkoroi ikiwa ya pili kwa alama 98. Tatu bora zinafungwa na Nairobi Prisons kwa alama 97, tano mbele ya RVSA huku huku White Eagles ikitinga tano kwa alama 80.

 
 
bottom of page