Kariobangi Tayari Kutuzwa Mabingwa wa Taji la NERL
- heartmediak4
- Aug 20, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 20 Agosti 2024

KARIOBANGI Legends Youth imekaa mkao wa subira kutawazwa wafalme wa kampeni za FKF Kundi B Ligi ya Nairobi Mashariki (NERL) muhula huu. Kariobangi ya kocha, Geoffrey Wangalwa na Jeremiah Akhayo imepiga hatua hiyo baada ya kushinda mechi mbili kwa bao 1-0 kila moja dhidi ya Santos Hotspurs na Mathare North Youth. Mabao hayo yalitupiwa kimiani na Dennis Wafula. ''Bila shaka tunapongeza vijana wetu kwa kazi nzuri ambayo wamefanya kwenye kampeni za msimu huu,'' anasema kocha mkuu. Anaongeza kwamba wana furaha tele maana hatimaye wametimiza azma yao kutwaa tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki ligi ya taifa daraja ya pili muhula ujao.
Hata hivyo anashikilia kuwa wamepania kujituma kiume kuhakikisha wanashinda mechi tatu zilizosalia ili kukamilisha ratiba yao msimu huu. Kariobangi Legends kwa sasa inaongoza kwa kuzoa alama 103 baada ya kushuka dimbani mara 39 ambapo imefungia wapinzani wao kabisa wala hawawezi kuipiku. Kwa sasa timu zingine zinapigania kumaliza nafasi ya pili inayoshikiliwa na Lucky Summer ya kocha, Dan Nguya iliyopiga Tumaini FC kwa mabao 3-0. Joel Arika ilitikisa wavu mara mbili huku Dennis Opiyo akifunga bao moja. ''Tayari ubingwa wa msimu huu umeenda sasa tunataka kumaliza kati ya nafasi ya pili bora ili kujiweka pazuri kutwaa tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya pili msimu ujao,'' anasema kocha wa Lucky Summer. Anaongeza kuwa ingawa zimesalia mechi nne ili kukamilisha ratiba yao kamwe hawawezi kudharau wapinzani wao maana kila timu imejituma kiume kwenye juhudi za kumaliza kati ya nafasi nzuri.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Babadogo United ilisajili ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Santos Hotspurs, Lula FC ilipigwa mabao 3-2 na Mathare North United, Wendani Allstars ilitoka mabao 2-2 na Hakati Sportiff nayo Pumwani Sportiff ilicharaza Utawala Youth mabao 2-0. Gor Mahia Youth ilicharaza Fortune Kinderen mabao 2-0 huku Automech ikitoka sare tasa na Rada Sports.


