top of page
Search

Kariobangi Legends Youth Msimu Mmoja NERL Umetosha

  • heartmediak4
  • Aug 13, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 13 Agosti 2024


KARIOBANGI Legends Youth inahitaji kushinda mchezo mmoja ili kukaa mkao wa kula ikisubiria kutawazwa mabingwa wa kampeni za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) muhula huu. Huku ikiwa zimesalia mechi tano kukamilisha ratiba ya msimu huu, Kariobangi ya kocha, Geoffrey Wangalwa na Jeremiah Akhayo inazidi kutesa wapinzani wao. Timu hii iliyoasisiwa mwaka uliyopita inahitaji kushinda mechi moja na kuzoa alama tatu ili kufungia mahasimu wao Lucky Summer. ''Katika mpango mzima tunapongeza wachezaji wetu kwa kazi nzuri walioshusha kwenye kampeni za muhula huu,'' anasema kocha mkuu. Anaongeza kuwa ana imani vijana wake wanatosha mboga pia wapo tayari kumaliza biashara kesho Jumatano tarehe 14 Agosti watakapocheza na Santos Hotspurs.




Kariobangi imefikia hatua hiyo baada ya kunyamazisha Gunners kwa mabao 3-0 mwishoni mwa wiki. Kikosi hicho kilipata ufanisi huo kupitia juhudi zao Ian Onyango, Bramwel Kavaya na Idris Amadi waliotikisa wavu mara moja kila mmoja.

Nayo Lucky Summer ya kocha, Dan Nguya iliangusha Umoja Rhinos kwa mabao 6-0 na kuendelea kushikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa kipute hicho. ''Tunaendelea vizuri kwenye kampeni zetu ambapo kwa sasa tumepania kumaliza nafasi ya pili na kutwaa tiketi ya kupanda ngazi maana tayari taji limeenda na wapinzani wetu,'' anasema kocha wa Lucky Summer. Anashikilia kwamba kampeni za msimu huu zimeshuhudia ushindani mkali kinyume na michuano ya muhula uliyopita.

Mabao hayo yalipatikana kupitia Joel Arika aliyepiga 'hat trick,' Dicklark Wafula, Denis Opiyo na Kennedy Ongalo ambao kila mmoja alitikisa wavu mara moja.

Babadogo United ilijiongezea alama tatu baada ya kuadhibu Tumaini FC kwa magoli 2-0. Kariobangi ingali kifua mbele kwa alama 97 nayo Lucky Summer inakamata mbili bora kwa kuzoa pointi 80, sita mbele ya Babdogo United.






Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Lula FC ilipigwa mabao 2-1 na Santos Hotspurs. Naye Stephen Ajode alicheka na wavu mara mbili na kusaidia Automech kutoka nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya Fortune Kinderen.

Gor Mahia Youth iliona giza ilipozabwa mabao 2-0 na Wendani Allstars, Mathare North Youth ilichapa Utawala Youth mabao 2-1. Tena United ilitoka nguvu sawa 0-0 na Soweto Allstars huku UEFA Despanol na Pumwani Sports kila moja ikisajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Ruai United na Rada Sports mtawalia.


 
 
bottom of page