top of page
Search

Kariobangi Legends Youth, Lucky Summer Nomaree Mechi za NERL

  • heartmediak4
  • Jul 24, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumatano, 24 Julai 2024


KARIOBANGI Legends Youth na Lucky Summer Sports zinazidi kutesa kwenye kampeni za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL). Kariobangi Legends Youth ya kocha, Geoffrey Wangalwa na Jeremiah Akhayo



ilibeba alama sita baada ya kupiga mechi mbili wikendi. Vijana hao waliangusha Soweto All Stars kwa mabao 6-0 kisha ilidunga Gunners FC bao 1-0. Kwenye mechi ya Gunners bao hilo lilifungwa na Dennis Wafula. Kwenye mchezo wa pili, Bramuel Kavaya alipiga 'hat trick' nao Dennis Wafula, Ian Onyango na Prise Luvutse kila mmoja alitikisa wavu mara moja. ''Bila shaka tunazidi kupiga hatua kwenye kampeni zetu ambapo kwa sasa tumeweka pengo la alama tisa dhidi ya mahasimu wetu na tumepania kuendeleza mtindo huo,'' anasema Geoffrey Wangalwa. Anaongeza kuwa vijana wake hawana lingine bali lazima wajitume kiume kufukuzia tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki ligi ya taifa Daraja la pili msimu ujao.


Naye kocha, Dan Nguya aliongoza, Lucky Summer kubeba ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Babadogo United. Lucky Summer ilipata ufanisi huo kupitia juhudi zake Gideon Omondi na Rijakaard Otieno huku Alex Ochieng akifungia Babadogo bao la kufuta machozi. ''Tunafanya vizuri lakini bado tunakabiliwa na mtihani mgumu mbele ya wapinzani wetu,'' anasema kocha wa Lucky Summer.

Naye meneja wa Babadogo, Ben Wanjala amekubali kushindwa kwenye mechi hiyo na kusema ni pigo kubwa kwenye kampeni zao. ''Tumekubali yaishe maana vijana walijituma kiume lakini bahati haikusimama kwenye mechi hiyo sasa tunapiga hesabu ya michuano ijayo,'' anasema. Anaongeza kuwa licha ya kudondosha alama tatu kwenye patashika hiyo bado hawajavunjika moyo wamepania kuendelea kupambana mwanzo mwisho.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Wendani Allstars iliona giza iliponyukwa mabao 3-2 na Pumwani Sports, Mathare North Youth ilizaba Fortune Kinderen kwa bao 1-0, Lula FC ililala kwa bao 1-0 mbele ya Umoja Rhinos nayo Hakati Sportiff ilidunga Tumaini FC bao 1-0.



Nazo Mathare North United na Gunners kila moja ilibeba ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Automech FC na Rada Sports mtawalia. Ruai United iliraruliwa kwa mabao 3-1 na Utawala Youth, Tena United ilipigwa bao 1-0 na UEFA Despanol nayo Santos Hotspurs ilitoka nguvu sawa bao 1-1 dhidi ya Gor Mahia Youth.

Baada ya matokeo hayo, Kariobangi Legends Youth ingali kifua mbele kwa kuzoa alama 79, tisa mbele ya Lucky Summers kwa kucheza mechi 31 na 32 mtawalia. Utawala Youth inashikilia tatu bora kwa alama 66, mbili mbele ya Babadogo United.

 
 
bottom of page