top of page
Search

Kariobangi Legends Youth Kutifua Vumbi Dhidi ya Utafiti Daraja la Pili

  • heartmediak4
  • Nov 1, 2024
  • 1 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 1 Novemba 2024




MECHI za Kundi C kuwania Ligi ya Taifa Daraja la Pili wikendi hii zinaingia raundi ya nne ambapo patashika saba zimepangwa kuchezwa kwenye viwanja tofauti. Jumamosi hii tarehe 2 Novemba 2024, Royal Fresh FC itakaribisha Tusker Youth ugani Kiriti Stadium. South C Rangers itakuwa kiamboni kualika Blue Nile uwanjani MOW South C, nayo Kariobangi Legends Youth itasafiri ugani Kari Kikuyu kucheza na wenyeji wao Utafiti.

South C Rangers inashikilia nafasi ya pili kwa kuzoa alama sita baada ya kushinda mechi mbili na kudondosha patashika itakuwa kazini kupigania alama tatu muhimu.

Katika msimamo wa mechi hizo, Shofco inaongoza kwa alama tisa baada ya kushinda patashika tatu ambazo imeshiriki.



Nayo Kariobangi Legends Youth inayojivunia kushinda mechi moja ambayo imeshiriki inalenga kushinda patashika hiyo ili kupanda hatua kadhaa katika jedwali. Kariobangi ilipandishwa ngazi baada ya kufanya kweli kwenye mechi za Ligi ya Kanda ya Nairobi. Kikosi hicho kinajivunia wachezaji wake mahiri akiwamo Laurence Otieno (nahodha), Bramwel Kavaya, Dennis Murigi, Victor Kunyili na Fidel Mwanzia kati ya wengine.


''Tuna imani tumeandaa wachezaji thabiti kukabili wapinzani wetu kwenye mechi hiyo,'' anasema mwenyekiti wa Kariobangi, Eric Otieno Atanga, Anaongeza kwamba ushindi wao utazidi kuwatia motisha zaidi kwenye michuano ya msimu huu wanayoshiriki kwa mara ya kwanza. Kariobangi inashikilia nafasi ya tisa kwa alama tatu, sawa na Embakasi United pia Githurai All Stars tofauti ikiwa idadi ya mabao.



Katika ratiba ya Jumapili tarehe 3, Novemba 2024, Gikuni United itaumana na Thika Sports, Tatu City itapepetana na Kikuyu Township, Githurai All Stars itamenyana na Nyahururu Griffons huku Sunsine FC ikikutanishwa na Embakasi United.

 
 
bottom of page