Kariobangi Legends Youth Kukabili Gikuna Kwenye Ufunguzi wa Daraja la Pili
- heartmediak4
- Oct 12, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Jumamosi, 12 Oktoba 2024

JUMLA ya mechi tano zimeratibiwa kuchezwa Jumapili hii tarehe, 13 Oktoba 2024 kwenye ratiba ya michuano ya Kundi C katika Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu huu. Kariobangi Legends Youth inayoshiriki kipute hicho kw amara ya kwanza itakuwa inafungua kampeni zake dhidi ya Gikuna United katika uga wa kiamboni, Kariobangi Primary, Embakasi, Nairoibi. Kikosi hicho kina imani kitaanza mbio zake vyema. Kariobangi Legends Youth itakuwa chini kocha mpya, Osborne Monday baada ya Geoffrey Wangalwa kupigwa kalamu. ''Tuna imani tumeandaa vijana wetu vizuri na tayari kufanya kama walivyofanya kwenye mechi za Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) msimu uliyopita,'' anasema mwenyekiti wake, Eric Atanga Otieno. Anaongeza itakuwa muhimu wachezaji wake kushiriki mchezo huo wakiwa makini zaidi maana pande zote zitakuwa zikisomana. Pia itakuwa mara ya kwanza timu hizo kukutana. Kwenye ratiba hiyo, Nyahururu itacheza na Sunshine, Thika Sporting itachuana na South C Rangers, Utafiti itapepetana na Royal Fresh nayo Kikuytu Town ship itaumana na Blue Nile.
Kariobangi Legends Youth inajivunia kunasa huduma za wachezaji nane wapya wakiwamo: Rivaldo Seda (Nyakango), James Karanja (Santos Hotspurs), Yahya Mwai (Kariobangi Sports), Paul Odhiambo (Acakoro), Romeo Mafuta (Hakati Sportiff), Kent Babu (RYSA), Abdalla Siraji na Alvin Odari kutoka Soweto Allstars na Laiser Hill Academy mtawalia.
Baada ya msimu uliyopita kukamilika klabu hii iliwaonyesha mlango wachezaji wafuatao: Moving Omondi. Peter Kepher, Milton Ouma, Michael Okoth, Yusuf Baboya, Eugene Mutava na Tom Bonface.


