Kariobangi Legends Wazee Yazamisha Babadogo Wazee Japo Kirafiki
- heartmediak4
- Sep 10, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 10 Septemba 2024
TIMU ya Kariobangi Legends Wazee imeendeleza ubabe wake baada ya kuidunga Babadogo Wazee kwa mabao 4-1 kwenye mchuano wa kirafiki uliochezwa Jumapili tarehe 8, Septemba 2024 ugani Kariobangi Primary.
Kariobangi Legends Wazee ni kati ya vikosi ambavyo hushiriki Ligi ya Wazee Pamoja Kanda ya Nairobi mwaka 2024.

Kariobangi Legends Wazee ya kocha, Philip Munyoki ilitembeza soka safi na kuhakikisha imetwaa ufanisi wa pointi tatu japo kirafiki. Kariobangi ilivuna ushindi huo kupitia Hillary Otieno aliyepiga 'hat trick' naye Vincent Opondo alitikisa wavu mara moja. Babadogo Wazee ilipata mabao ya kufutia machozi kupitia juhudi zake Brian Otieno na Martin Makango.
''Kama kawaida tulionyesha soka ya kupendeza na kuhakikisha tumezima wapinzani wetu,'' anasema kocha wa Kariobangi Legends Wazee. Anaongeza kuwa wamepania kuendeleza ubabe wao dhidi ya wapinzani wao maana wanatosha mboga dimbani. Naye Vickson Nzomo wa Babadogo Wazee alikubali yaishe na kusema wanazidi kujifunza soka kila wakati wanashiriki mechi za ligi ama za kupimana nguvu.

Kariobangi Legends inategemea wachezaji shupavu ikiwamo Erick Atanga Otieno maarufu Sunga (nahodha), Philip Munyoki maarufu Pinto, Hillary Otieno maarufu Koreo na Geoffrey Wangalwa maarufu Gae. Ligi ya wazee inashirikisha timu kama ABSA Legends mabingwa watetezi baada ya kubeba taji hilo msimu uliyopita. Timu zingine ni Jambo Fc, Tipples FC, Comrades FC, Soul Lounge FC, Dandora Evergreen Legends na Wazee Hatari.


