Kariobangi Legends Wazee Inazidi Kurarua Wapinzani Wao Japo Kirafiki
- heartmediak4
- Oct 11, 2024
- 1 min read
Na HERAT MEDIA
Ijumaa, 11 Oktoba 2024.

KARIOBANGI Legends Wazee inazidi kutetemesha wapinzani wao kwenye mechi za kirafiki huku wachezaji wake wakiashiria kwamba wana uwezo wa kuibuka mabingwa wa ligi ya wazee katika Kaunti ya Nairobi. Ikiongozwa na kocha, Philip Munyoki timu hiyo iliangusha Mathare North Legends kwa mabao 6-1 kwenye mechi iliyochezewa uga wa Drive Inn Primary, Mathare North.
Kwenye michuano mingine iliyochezwa mwishoni mwa mwezi uliyopita, wanasoka hao walipiga Thika Vitambi Wazee kwa mabao 4-3 mjini Thika, walitoka sare tasa na The Board. Hata
hivyo walijikuta kwenye wakati mgumu walipozabwa mabao 4-3 na Dandora Old Boys.

''Bila shaka ninapongeza wenzangu kwa kazi nzuri tunaozidi kuonyesha kwenye mechi zetu,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kuwa ufanisi wao unachangiwa pakubwa na jinsi wanavyotuma kwa udi na uvumba licha ya kwamba baadhi yao wana umri mkubwa jambo linalowafanya kuwa vigumu kusakata kabumbu vizuri.
Anashikilia kuwa wanalenga kuendeleza ubabe huo dhidi ya wapinzani wao maana wanatosha mboga dimbani. Kariobangi Legends inategemea wachezaji shupavu akiwamo Erick Atanga Otieno maarufu Sunga (nahodha), Philip Munyoki maarufu Pinto, Hillary Otieno maarufu Koreo na Geoffrey Wangalwa maarufu Gae. Ligi ya wazee inashirikisha timu kama ABSA Legends mabingwa watetezi baada ya kubeba taji hilo msimu uliyopita. Timu zingine ni Jambo Fc, Tipples FC, Comrades FC, Soul Lounge FC, Dandora Evergreen Legends na Wazee Hatari FC.



