Kariobangi L. Youth Yataka Kushinda Mechi 4 Ifungie Mahasimu wao Mbio za Kipute cha NERL
- heartmediak4
- Aug 7, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumatano, 7 Agosti

WACHANA nyavu wa Kariobangi Legends Youth wanahitaji kushinda patashika nne ili kuhakikisha wameibuka mabingwa wa kampeni za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) msimu huu. Wakishinda mechi hizo kati ya nane ambazo zimesalia watafungia mahasimu wao Lucky Summer.
Kariobangi inaongoza kwa alama 88 nayo Lucky Summer ni ya pili kwa alama 77 huku zikiwa zimesalia mechi nane na saba mtawalia. Ushindi wa mechi nne utaibeba Kariobangi kufikisha alama 100 nayo Lucky Summer ikishinda mechi zote saba itakusanya alama 98.
''Kwa jinsi vijana wangu wanavyoshusha soka la kibiashara sina shaka kutaja kuwa lazima tubeba ubingwa na kupandishwa ngazi,'' anasema kocha wa Kariobangi, Geoffrey Wangalwa. Anaongeza kuwa katika mpango mzima wamepania kushinda mechi zote zilizosalia ingawa wanahitaji ushindi wa mechi nne ndio wazime juhudi za wapinzani wao.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Eric Atanga Otieno anawapigia chapuo vijana hao wamejitume kisabuni na wahakikishe wamezoa tiketi ya kupandishwa ngazi msimu ujao. ''Kusema ukweli binfasi sina lingine bali nataka tiketi ya kusonga mbele hatupo tayari kushiriki ngarambe ya NERL kwa mara ya pili maana vijana wanatosha mboga,'' anasema. Anaongeza baada ya kutazama wachezaji wake jinsi wanavyosakata kabumbu hawana sababu yoyote ya kutotimiza azma yao.
Kariobangi Legends Youth inategemea wapigagozi hodari kama Dennis Wafula, Bramuel Kavaya, Ian Onyango (nahodha), Prise Luvutse, Victor Kinyuli, George Karani, Tom Bonface na Lawrence Otieno.

''Kazi ipo lakini hatuna shaka lazima tupambane kufa na kupona kwenye jitihada za kuwania kumaliza kileleni kwenye kampeni za muhula huu,'' anasema kocha Lucky Summer, Dan Nguya. Anatoa wito kwa vijana wake kutolaza damu dimbani kwenye mechi zilizosalia.
Lucky Summer inajivunia huduma za wachana nyavu kama Dennis Opiyo, Levis Odede, Rijkaard Otieno na Joel Arika kati ya wengine. Katika msimamo wa ngarambe hiyo, Babadogo United imesajili alama 71 na kufunga tatu bora nayo Utawala Youth inashikilia nafasi ya nne kwa alama 69, sita mbele ya Automech FC.


