Kahliweed, Kayole Select Zatinga Raundi ya 16 Bora Kipute cha Kothbiro
- heartmediak4
- Sep 18, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Alhamisi, 18 Septemba 2024
TIMU ya Kahliweed FC na Kayole Select zinajiandaa kutifua vumbi kwenye mechi za raundi ya 16 bora za makala ya 47 kuwania taji la Kothbiro. Kahliweed na Kayole kila moja ilimaliza mechi za mchujo kibabe kwa kuvuna mabao 2-1 na 2-0 dhidi ya Leads United na Napoli FC mtawalia ugani Umeme Ziwani, Nairobi Jumatatu, 16 Septemba 2024.

Kwenye mechi za Kundi A, Kahliweed ya kocha, Henry Mitcho ilipata ufanisi huo kupitia juhudi zake Kevin Omondi na Musa Mwangi. Naye Henry Api alifungia Leads United bao la kufutia machozi. ''Ndio mara ya pili tunashiriki ngarambe hii ambapo tumepania kubeba kombe la mwaka huu,'' alisema kocha wa Kahliweed. Aliongeza kuwa ni muda mrefu tangia timu kutoka mtaani Ziwani ibeba taji hilo. Anashikilia kuwa wamejipanga kuonyesha wapizani wao kuwa mtaa huo una wachezaji wenye talanta katika mchezo wa soka.

Kwenye patashika nyingine, Maleche Ali alitikisa wavu mara mbili huku Ochola Salim akipiga kombora moja na kusaidia Kamkunji Falcons kuvuna mabao 3-0 mbele ya Biafra Kamaliza.
Mabao ya Kayole Select yalipatikana kupitia Steve Orland na Francis Nambute. Katika msimamo wa Kundi A, Leads United na Kahliweed zimesonga mbele kwa kuzoa alama sita na tano mtawalia. Kundi D, Kayole Select imeibuka kileleni kwa alama saba, mbili mbele ya Black Mamba iliyosajili ushindi wa mezani baada ya Macmilan Senior kuingia gizani.

Katika ratiba ya mechi ambazo zimepangwa kuchezwa Jumatano hii tarehe 18, Septemba 2024 Kundi F, Eastleigh Stars itakabili Kiambiu Warriors nayo Ziwani All Stars itachuana na Pumwani Sports Club. Kundi H, Mathare Commban itakutanishwa na Pangani United. Katika jedwali la Kundi F, Ziwani All Stars inaongoza kwa alama nne sawa na Pumwani Sports tofauti ikiwa idadi ya mabao. Kiambiu Warriors inashikilia nafasi ya tatu kwa alama mbili nayo Eastleigh Stars ya mwisho bila alama.
Pumwani Sports ndio mabingwa watetezi. Kwenye mechi za makala ya 44 Leads United ilimaliza ya pili iliponyukwa mabao 4-2 na Korongez kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali. Kwenye makala ya 45 mshindi alikosekana kufuatia hatua ya wafuasi wa Borussia FC kuzua fujo baada ya kikosi hicho kutoka sare tasa na Leads United katika fainali.


