Handiboli: NCPB, Equity Bank Zajitosa Fainali Super Cup
- heartmediak4
- Aug 6, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 6 Agosti 2024
TIMU ya wanaume ya handiboli ya Halmashauri ya Nafaka na Mazao nchini (NCPB) imeadhibu Kenya General Service Unit (GSU) kwa magoli 35-26 kwenye nusu fainali za kuwania taji la Super Cup zilizopigiwa ugani Ulinzi Complex, Lang'ata Nairobi. Nao waliokuwa mabingwa watetezi Maafande wa Jeshi la Ulinzi (KDF) wamejikuta njia panda walipozabwa mabao 20-19 Equity Bank kwenye mechi zilizochezwa Jumapili tarehe 4, Agosti.

NCPB ilipigwa jeki pakubwa kupitia juhudi zake Timothy Kirimi na Nicholas Okore waliofunga mabao 13 na kutikisa wavu mara nne.
Nao wachezaji wa GSU ambao hutiwa makali na kocha, Joseph Okwema walijituma kiume ambapo Philip Oscar alifunga mabao kumi. Nao Elton Esara na Stephen Wanyonyi kila mmoja alitikisa wavu mara tano.
KDF ya kocha, Nixon Oyaro ilishindwa ujanja huku Kevin Imo na Gideon Kiprotich wakiibuka bora kwa kucheka na wavu mara sita na nne mtawalia.
Upande wa Equity Maxwell Munene alitupia kimiani mabao manne nao Rashid Inguela na Brian Wakhuka kila mmoja alitetemesha wavu mara tatu.

''Vijana wangu walijituma kwa udi na uvumba na kushinda mechi za mchujo pia nusu fainali sasa tunapiga hesabu ya fainali ambapo tuna imani haitakuwa mteremko,'' anasema kocha wa NCPB, Brian Mathew. Aliongeza kuwa lazima wawe makini wasije wakarejelea makosa waliofanya msimu uliyopita. Muhula uliyopita NCPB ilipokonywa taji hilo na KDF iliyoinyamazisha katika fainali.
Kocha wa GSU alikubali yaishe na kuhaidi kupambana zaidi kwenye mechi za ligi kuu msimu ujao.
NCPB ilifuzu kwa nusu fainali baada ya kumaliza kileleni Kundi A kwa kuzoa alama nne, mbili mbele ya Equity Bank. Nayo GSU ilikuwa imeibuka ya pili Kundi B kwa kusajili alama mbili.KDF ilimaliza kifua mbele Kundi B kwa kuzoa alama nnE.
Kwenye mechi za kina dada, Malkia wa mchezo huo nchini, Jeshi la Ulinzi (KDF) maarufu Ulinzi Sharks walipiga Rangers kwa mabao 28-16. Nayo NCPB ilinyukwa mabao 29-27 na Nairobi Water Queens


