Handiboli: Equity Bank, KDF Zatetemesha Taji la Super Cup
- heartmediak4
- Aug 13, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 13 Agosti 2024.
MASHINDANO ya handiboli kuwania taji la Super Cup makala ya mwaka huu yalishuhudia ushindani mkali kuliko miaka iliyopita ambapo yalipata mabingwa wapya kitengo cha wanaume na wanawake. Timu ya wanaume ya Halmashauri ya Nafaka na Mazao nchini (NCPB) iliyokuwa imeshinda mara tatu na Jeshi la Ulinzi (KDF) iliyokuwa bingwa mtetezi kila moja iliona giza ambapo washiriki wapya Equity Bank waliibuka wafalme wapya.

Kwa kina dada Jeshi la Ulinzi (KDF) maarufu Ulinzi Sharks ilitazwa malkia baada ya kuzima Nairobi Water Queens iliyokuwa mabingwa watetezi.
KDF ya kocha. Nixon Oyaro ilipiga waliokuwa mabingwa watetezi, Nairobi Water Queens kwa mabao 29-26 katika fainali kali ugani Ulinzi Complex, Langata Nairobi. Sharon Mulei na Sarah Wasike wote wa KDF waliibuka wafungaji Bora baada ya kucheka na wavu mara Saba Kila mmoja. Upande wa Nairobi Water wafungaji Bora walikuwa Merina Andala na Tracy Awino waliotikisa wavu mara nane na sita mtawalia. "Bila shaka tunapongeza wachezaji wetu kwa ufanisi huo hasa baada ya Wanaume kukosa tiketi ya fainali," alisema meneja wa KDF, Yusuf Kipkoech. Aliongeza kuwa ulikuwa mchezo rahisi maana walikuwa wamekomoa wapinzani hao kwenye mechi ya mwisho ya ligi kuu msimu uliyopita.

Equity Bank ya kocha, Peter Mwathi na Tyrus Ochieng ilikuwa imeshusha ushindani mkali kwenye kampeni za ligi huku ikipania kuibuka kati ya nafasi sita bora ili kushiriki Super Cup.
''Katika fainali tulifahamu bayana tuna kibarua kigumu lakini wachezaji wetu walikuwa makini licha ya wapinzani wetu kutoka chini kwa mabao matano na kutufikia,'' alisema kocha mkuu wa Equity Bank. Aliongeza kuwa walikuwa wamepanga kupambana kwa udi na uvumba kuhakikisha wametwaa taji hilo baada ya kulemewa kubeba ligi kuu. Equity Bank ilitawazwa mabingwa kwa kuzaba NCPB mabao 30-29 kwenye ukumbi wa Ulinzi Complex, Lang'ata Nairobi. Hadi kipindi cha mapumziko matokeo yalikuwa Equity Bank 15-12 NCPB kisha muda wa kawaida yalikuwa sawa Equity Bank 23-23 NCPB.
Timu hizo zilicheza muda wa zaidi wa dakika kumi ambapo zilimaliza nguvu sawa Equity 26-26 NCPB. Kisha ziliongezwa dakika zingine kumi ambapo hatimaye Equity Bank ilimaliza kifua mbele mabao 30-29 dhidi ya NCPB.

Wachezaji wa Equity Bank, Brian Wakukha, Maxwel Munene na Brian Murangiri walionyesha mechi ya kupendeza. Upande wa NCPB wachezaji bora walikuwa Robert Maranga, William Malui na Timothy Kirimi bila kusahau Snox Collins.
Kwenye tuzo za kibinafsi zilizoendea wanaume wa NCPB, kipa bora aliibuka Ian Odhiambo, William Malui aliibuka beki bora huku Timothy Kirimi akizoa tuzo ya winga wa kushoto. Kwa wachezaji wa Equity Bank, Brian Murangiri aliibuka mchezaji bora wa kushoto(left back) naye Brian Munene alibeba tuzo ya mchezaji bora wa katikati (centre back). Kwenye nusu fainali ya wanawake, Equity ilinyuka KDF kwa mabao 20-19 nayo NCPB ilibeba mabao 35-26 mbele ya Kenya General Service Unit (GSU).
Kwenye mechi za nusu za kina dada KDF ilipiga Rangers kwa mabao 28-16. Nayo NCPB ilinyukwa mabao 29-27 na Nairobi Water Queen Queens.


