top of page
Search

Gikuni United Mwanzo Mbaya Ligi ya Daraja la Pili

  • heartmediak4
  • Oct 15, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne 15, Oktoba 2024


GIKUNI United ilidungwa bao 1-0 na Kariobangi Legends Youth kwenye mechi za Kundi C katika kampeni za Ligi ya Taifa Daraja la Pili ugani Kariobangi North, Embakasi Nairobi, iliyochezwa Jumapili tarehe 13, Oktoba 2024. Nayo South C Rangers ya Nairobi ilirejea nyumbani kwa tabasamu baada ya kuadhibu wenyeji wao Thika Sporting ya Thika kwa mabao 4-1.



Gikuni United ya kocha, Joseph Makumi na Claude Sofa iliteremsha soka safi huku ikisaka alama tatu ugenini. Katika mpango mzima mlinda lango wa Gikuni United aliibeba na kuibuka shupavu kwa kuokoa mipira nyingi tu kwani Kariobangi Legends Youth ingepata ushindi wa mnono.


Kariobangi Legends Youth inayonolewa na kocha, Osborne Monday ilipata bao la pekee ndani ya kipindi cha pili kupitia juhudi zake Laurence Otieno. ''Ninapongeza vijana wangu kusajili alama tatu muhimu nyumbani ikiwa ndio mechi ya ufunguzi,'' anasema mwenyekiti wake, Atanga Eric Otieno.


Anaongeza wangepata ushindi mkubwa jinsi walivyozoea lakini uchofu uliponda. wachezaji wake. Anashikilia kuwa vijana wake hawakupata muda wa kupumzika vizuri wakati ligi ilikamilika. Anadokeza kwamba pia vijana hawajazoeana dimbani baada ya kutema wachezaji saba na kuleta idadi sawa.

Kadhalika anahisi vijana hao bado hawajaelewa mbinu za kocha mpya baada waliyekuwa wamezoea kuondoka. Ni mechi ya kwanza ya ligi kocha huyo kuongoza vijana hao ambapo anasema ushindi huo unawapa motisha pakubwa licha ya kupoteza nafasi kadhaa wangefunga mabao zaidi. ''Kwanza sina pupa nimepania kukabili kila mechi kwa wakati wake lakini tukipania kufanya kweli tena ndio mwanzo wa ngoma kupiga soka la Daraja la Pili,'' Monday anasema. Anaongeza wanayo fursa ya kujituma kiume na kuonyesha ubabe wao kama wanavyokusudia.

Kariobangi na Gikuni zinashiriki kipute hicho baada ya kupandishwa msimu uliyopita kutoka ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki na Ligi ya kanda ya Kati mtawalia. Nayo Royal Fresh FC ilituzwa ushindi wa mezani baada ya wenyeji wao Utafiti FC kusepa na kuingia gizani. Nyahururu Griffons ilicharazwa mabao 2-0 na Sunshine, Shofco iliangusha Embakasi United kwa mabao 2-0 huku Kikuyu Township ilitoka nguvu sawa mabao 2-2 na Blue Nile FC.




Matokeo mengine Kundi A: Thika Stars 0-3 Delmonte FC, Lucky Summer 0-0 Police Youth, Butterfly 2-2 Thika Sharks, Kirigiti Community 1-2 Kangemi Allstars, Jumbo T 0-1 Nkoroi.

KUNDI B: Juja Community 0-2 Thika Cloth Mills, Vision FC 0-0 Thunderbirds.

KUNDI D: Enkasiti FC 4-2 Panther FC, Othaya Greensantos 0-2 Aspire Nyahururu.

 
 
bottom of page