top of page
Search

Gikuni, Kariobangi Legends Youth Kila Moja Mzigoni Daraja 2

  • heartmediak4
  • Oct 19, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumamosi, 19 Oktoba 2024




KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa kwenye mechi za Kundi C kufukuzia taji la Ligi ya Taifa Daraja la Pili wikendi hii. Gikuni United Jumapili hii tarehe 20 Oktoba itachuana na Nyahururu Griffons. Gikuni ya kocha, Joseph Makumi itakuwa mbioni kulipiza kisasi baada ya kuzabwa bao 1-0 na Kariobangi Legends Youth. ''Tumeandaa wachezaji wetu tayari kukabili wapinzani wetu lengo likiwa kubeba alama tatu muhimu baada ya kufungua kampeni zetu vibaya,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kuwa wanaamini wachezaji wao wameiva na tayari kutesa kwenye kampeni za muhula huu. Kwenye ufunguzi wa mechi za kipute hicho, Nyahururu Griffons ilicharazwa mabao 2-0 na Sunshine.


Nayo Kariobangi Legends Youth inayotiwa makali na Osborne Monday itakuwa ugenini katika uga wa Kiriti kuchuana na wenyeji wao Royal Fresh. ''Tumepania kujituma kwa udi na uvumba kuhakikisha tunabeba ushindi wa alama zote ili kuendelea kupata motisha zaidi kwenye kampeni za msimu huu,'' anasema kocha wa Kariobangi Legends Youth. Anaongeza kwamba wachezaji wake wana kiu cha kufanya kweli kwenye michuano ya ligi mpya. Mwenyekiti wa klabu hiyo, Eric Atanga Otieno anasema vijana wake wamekaa vizuri kufanya kweli kwenye patashika hiyo. ''Tumepania kukaza buti kwenye mechi zetu kuhakikisha tutafanya kweli na kunasa tiketi ya kupandishwa ngazi msimu ujao,'' anasema mwenyekiti huyo. Kariobangi Legends Youth inategemea huduma za wachezaji shupavu kama Laurence Otieno (nahodha), Bramwel Kavaya, Dennis Murigi, Victor Kunyili na Fidel Mwanzia kati ya wengine. Royal Fresh ilituzwa ushindi wa mezani baada ya Utafiti FC kuingia mitini.



Kwenye ratiba hiyo, Sunshine FC itachuana na Tusker Youth, Tatu City itapepetana na Thika Sporting, South C Rangers itamenyana na Embakasi United, Shofco itaumana na Kikuyu Township nayo Githurai All Stars itakutanishwa na Utafiti FC.

 
 
bottom of page